‎Chamwino, Dodoma

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza ujenzi wa daraja la Mto Msanjila linalojengwa katika Barabara ya Handali – Nghahelezi – Chitemo wilayani Chamwino mkoani Dodoma likilenga kurejesha mawasiliano na kurahisisha usafiri kati ya wilaya ya Chamwino na Mpwapwa.

‎Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Chamwino, Mhandisi Richard Sanga ambapo amesema ujenzi wa daraja hilo ulianza mwezi Septemba 2026 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2027.

‎Amesema daraja hilo linajengwa baada ya daraja la awali kuharibika kutokana na mvua hali iliyosababisha changamoto kubwa kwa wananchi wa kata ya Handali wilayani Chamwino na kata ya Mima wilayani Mpwapwa hususan katika usafiri, biashara na huduma za kijamii.

‎”Daraja hili ni kiunganishi muhimu kwa wananchi wa Chamwino na Mpwapwa, tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha za ujenzi wa daraja hili ambalo litasaidia kurejesha mawasiliano na kurahisisha usafiri na usafirishaji”, amesema Mhandisi Sanga.

‎Ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 15 huku kazi zinazoendelea kwa sasa zikihusisha umwagaji wa zege pamoja na ufungaji wa nondo kwa ajili ya msingi na kuta za daraja.

‎Kwa mujibu wa Mhandisi Sanga daraja hilo likikamilika litakuwa na urefu wa mita 43 na midomo nane huku likijengwa na mkandarasi Helian Investment Limited.

‎Naye, Diwani wa kata ya Nghahelezi Mhe. Joseph Ngomoko ameishukuru serikali kwa kuanza kuwajengea daraja hilo akisema kuharibika kwa daraja la awali kumeleta athari kubwa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

‎Amesema wakati wa mvua wagonjwa wamekuwa wakipata ugumu kufika katika hospitali ya Mvumi huku shughuli nyingine za wananchi zikikwama kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika.

‎”Daraja hili likikamilika litasaidia wagonjwa kufika hospitalini bila changamoto huku shughuli za kiuchumi zikiendelea bila vikwazo”, amesema.

‎Kwa upande wake, Bi. Evalina Masima mkazi wa Nghahelezi amesema kuharibika kwa daraja hilo kumepunguza kasi ya shughuli za maendeleo katika vijiji vyao na maeneo jirani kutokana na changamoto ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

‎Amesema magari yamekuwa yakishindwa kufika kwa urahisi katika maeneo hayo hali iliyowaathiri wafanyabiashara na wakulima wanaohitaji kusafirisha bidhaa zao kwenda mijini lakini daraja likikamilika watapata fursa ya kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi, kufanya biashara na kuongeza kipato.

‎Bw. Elias Msamvule mkazi wa Nghahelezi amesema mvua zinaponyesha mawasiliano kati ya kijiji cha Chinoje kilichopo Chamwino na vijiji vya Mima na Chitemo vilivyopo Mpwapwa yanakatika kutokana na hali ya daraja hilo.

‎Ameishukuru serikali kwa kuanza ujenzi wa daraja jipya litakalosaidia shughuli za kijamii na kiuchumi na ameomba ujenzi wa daraja hilo ukamilike kwa wakati ili wananchi waweze kuondokana na adha ya usafiri na usafirishaji iliyodumu kwa muda mrefu.