Mawakili wa Serikali wamefunzwa na wametakiwa kuzingatia taratibu na misingi ya kisheria ya kuandaa Hati za Makubaliano (Settlement Agreements) pale migogoro inayoihusu Serikali au taasisi zake inapokuwa imetatuliwa kwa njia ya Majadiliano au Suluhu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Majadiliano na Utatuzi wa Migogoro Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali *Bw. Benno Anthony Sanga* katika mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali katika Wiki ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara Tanzania na Mkutano wa Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara 2026 unaofanyika kuanzia tarehe 28 Septemba hadi tarehe 2 Oktoba, 2026 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu namna ya kuandaa hati za makubaliano ya mgogoro uliotatuliwa, Bw. Sanga aliwakumbusha Mawakili wa Serikali kuzingatia sheria kanuni na taratibu, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa wakati wa uaandaji wa Hati za Makubaliano.

Aidha, Bw. Sanga ameeleza kuwa ni muhimu Mawakili wa Serikali, kuihusisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kila hatua za majadiliano na uandaaji wa hati za makubaliano,ikiwa ni pamoja na kuziwasilisha hati hizo ziweze kufanyiwa upekuzi wa kina na kutolewa ushauri au mwongozo.  

Ameeleza kuwa, taasisi zikifuata hatua sahihi na kupata mwongozo kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutasaidia kuzuia kuibuka kwa migogoro katika hati hizo na kuipunguzia Serikali Hasara za kifedha.

Vilevile, Bw. Sanga ameeleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeboresha na kuimarisha ufanisi katika masuala ya Majadiliano na Utatuzi wa Migogoro, ambapo katika mwaka wa fedha wa 2026/27 imeanzisha Divisheni mpya ya *Majadiliano, Usimamizi wa Mikataba na Utatuzi wa Migogoro (DCNMDR).*

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni miongoni mwa Wadhamini wa Wiki ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara Tanzania na Mkutano wa Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara 2026 unaoratibiwa na *Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC)* na kubeba kauli mbiu isemayo *“Kujenga Imani katika Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR): Kuimarisha Ufanisi, Upatikanaji na Ubunifu katika Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara”.*