Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) mara baada ya kuona huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na wataalamu hao katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Picha Na. 2 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo akimkabidhi Zawadi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda wakati wa ziara yake katika eneo la huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na ORCI katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Picha Na. 3 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na wataalamu wa afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) baada ya kutembelea eneo la utoaji wa huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma.
Picha Na. 4 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akisaini kitabu cha wageni wakati wa ziara yake katika eneo la huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na ORCI katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC). Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo. Picha na ORCI
……………
Na Mwandishi Maalumu – Arusha
29/09/2026 Mbunge wa Jimbo la Arusha na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa kusogeza huduma za uchunguzi wa saratani karibu na wananchi wa Arusha na kuwafikishia huduma hizo Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma wanaoshiriki mkutani jijini humo.
Makonda alitoa pongezi hizo jana jijini Arusha alipokuwa akizungumza kuhusu huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na ORCI katika Hospitali ya Kaloleni kwa wananchi, pamoja na huduma zinazotolewa kwa viongozi na watendaji wanaoshiriki Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika jijini humo chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Alisema hatua ya ORCI kuwasogezea wananchi huduma za uchunguzi imewapa fursa ya kupata huduma karibu na maeneo yao ya makazi huku ikiwasaidia wananchi kubaini hali zao za afya mapema bila kulazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam.
Makonda aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi kupima afya zao huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema ni muhimu katika kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.
“Unatoka tu kwenye mtaa wako kuja Kaloleni Hospitali, unapima bila malipo na ukibainika una tatizo unapata huduma. Huhitaji kusafiri kwenda Dar es Salaam kutafuta hoteli wala kulipa gharama za chakula,” alisema.
Alisema hatua ya ORCI kutoa huduma pia katika mkutano unaowakutanisha viongozi na watendaji wakuu ni muhimu kwa kuwa inawawezesha kupata huduma za uchunguzi wakati wakiendelea na majukumu yao.
Makonda alisema viongozi na watendaji wana majukumu makubwa katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali hivyo afya yao ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele.
Akizungumza kuhusu upimaji huo Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alisema taasisi hiyo imeamua kutumia fursa ya C-CEOs Forum 2026 kuwasogezea viongozi huduma za uchunguzi wa awali wa saratani na elimu ya afya.
Alisema hatua hiyo imelenga kuwahamasisha viongozi kutanguliza afya zao na kuwa mfano kwa jamii katika suala la uchunguzi wa mapema.
“Tumefanya hivi kwa makusudi kwa sababu tunajua hawa viongozi wako busy na shughuli za ujenzi wa Taifa. Wakati mwingine hawana nafasi ya kwenda hospitalini kwa ajili ya kuangalia afya zao mpaka wanapojisikia kuumwa,” alisema.
Dkt. Msemo ambaye pia ni daktari bingwa wa saratani alisema saratani inaweza kuwa bila dalili katika hatua za awali hivyo kufanya uchunguzi kwa wakati ni muhimu katika kubaini viashiria na kuchukua hatua mapema.
Alisema wale watakaobainika kuwa na viashiria vinavyohitaji uchunguzi zaidi watapatiwa ushauri na kupewa rufaa kwa ajili ya uchunguzi wa kina na matibabu kulingana na mahitaji yao.
Dkt. Msemo alisema huduma zinazotolewa katika mkutano huo ni sehemu ya juhudi za ORCI za kupanua wigo wa huduma za uchunguzi na elimu ya saratani nchini.
Alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani kwa wakati.
Aidha Dkt. Diwani alisema ORCI imeendelea kupanua huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Saratani cha Mbeya na mipango ya kuwa na kituo kingine cha huduma za saratani mkoani Arusha.
Alisema hatua hizo zinalenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
Dkt. Msemo aliwataka wananchi na viongozi kutumia fursa za uchunguzi wa afya na kutosubiri hadi dalili za ugonjwa zitokee.
Mwisho
Picha Na. 1 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) mara baada ya kuona huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na wataalamu hao katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Picha Na. 2 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo akimkabidhi Zawadi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda wakati wa ziara yake katika eneo la huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na ORCI katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Picha Na. 3 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na wataalamu wa afya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) baada ya kutembelea eneo la utoaji wa huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma.
Picha Na. 4 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda akisaini kitabu cha wageni wakati wa ziara yake katika eneo la huduma za uchunguzi wa saratani zinazotolewa na ORCI katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC). Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo.
Picha na ORCI
