Na Victor Masangu, Kibaha

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amewaagiza wenyeviti wote wa serikali za mitaa pamoja na mabalozi kuhakikisha kwamba wanawahimiza wananchi wao kuachana kabisa na tabia ya kutupa taka hovyo pamoja na kusafisha mifereji na  kuzibua mitaro hasa katika  kipindi cha kuelekea   mvua kubwa za El- NINO  ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni katika baadhi ya maeneo.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake kuhusiana na namna ambavyo wamejiandaa na mvua hizo Mwenyekiti  Nyamka amebainisha kwamba katika kujiandaa na mvua hizo walikutana na baadhi ya viongozi mbali mbali wakiwemo wenyeviti hao pamoja na mabalozi ili kuweza kuweka mipango na mikakati ambayo itasaidia  katika kujikinga na El- NINO.
“Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA hivi karibuni ilitoa taarifa juu ya kuanza kwa mbua hizi kubwa za El- NINO na sisi kama chama tukaona ni vema tukutane na viongozi wetu mbali mbali kuanzia ngazi za chini ili kuweza kupeana maelekezo na majukumu ambayo yanapaswa kufanyika hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika mvua hizo na kikubwa tumewahimiza kutotupa taka hovyo,kuzibua mitaro pamoja na mifereji ili mvua inaponyesha maji yasiweze kukwama,”amebainisha Mwanyekiti Nyamka.

Pia amebainisha kwamba suala la TMA wameweza kulipokea kwa tahadhari kubwa sana na kwamba na wao  kama chama pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wameweza  kuzingatia maagizo na maelekezo yote ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa ngazi za juu katika kuhakikisha wananchi wanajiandaa  kikamilifu ili  kuepukana na  madhara ambayo yanaweza kujitokeza.

Kadhalika  Mwenyekiti Nyamka amewahimiza wananchi kuachana na kutupa taka hovyo na badala yake wale wote ambao watahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

katika hatua nyingine ameziomba  mamlaka zote zinazohusika kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo  Tarura na Tanrods   kuoana ni namna gani wanaweza kuhakikisha wanasimamia ipasavyo katika kufanya ukarabati  wa madaraja pamoja na makaravati ambayo yamekuwa ni hatarishi  hasa katika kipindi cha mvua zinaponyesha katika baadhi ya maeneo ikiwemo Kata  maeneo  ya  Muheza, Mwanalugali pamoja na maeneo mengine korofi

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) hivi karibuni walitangaza kuwepo kwa mvua kubwa za EL-Nino ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha katika baadhi ya   maeneo mbali mbali hapa nchini hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari za mapema ili kuepukanaa na madhara  na mafuriko ambayo yanaweza kujitokeza kutokana  na mvua hizo