Timu ya Michezo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (NJE Sports) imeshiriki uzinduzi rasmi wa Mashindano ya 40 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2026, yanayofanyika mkoani Kilimanjaro.

Mashindano hayo yakezinduliwa rasmi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, na yanafanyika chini ya kaulimbiu “Watumishi wa Umma Tuko Tayari kwa AFCON 2027.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Makonda amesema michezo ina nafasi muhimu kwa watumishi wa umma, si tu katika kuimarisha afya, bali pia katika kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Amesema mashindano hayo yanatoa fursa kwa watumishi kukutana, kushirikiana na kujenga mahusiano yatakayochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, Mhe. Makonda ameomba mashindano yajayo kufanyika mkoani Arusha, huku akihimiza kuendelea kuongeza thamani ya SHIMIWI kwa kuimarisha motisha na zawadi kwa washiriki, hususani zawadi za fedha taslimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewahakikishia wanamichezo na viongozi wanaoshiriki mashindano hayo kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umeweka mazingira salama na rafiki yatakayowawezesha kushiriki mashindano na kurejea katika maeneo yao salama baada ya kukamilika kwa mashindano.

NJE Sports inaendelea kushiriki michezo mbalimbali ya SHIMIWI 2026, ikiwa na dhamira ya kufanya vizuri, kuendeleza mshikamano miongoni mwa watumishi na kuiwakilisha vyema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.