Timu ya Mpira wa Miguu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG) imeanza vyema mashindano ya SHIMIWI 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Timu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mchezo huo umechezwa katika Uwanja wa CCP, Moshi, ambapo timu zote zilionyesha ushindani mkubwa katika kutafuta ushindi.

Bao pekee lililoamua mchezo huo lilifungwa dakika ya 52 ya kipindi cha pili na Michael Mhina, aliyemaliza pasi safi kutoka kwa nahodha John Mwakalebela, na kuipa timu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uongozi katika mechi hiyo.

Ushindi huo umeiwezesha timu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kujenga matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano hayo, huku wachezaji wakionyesha kiwango kizuri na mshikamano katika kipindi chote cha mchezo.

Mashindano ya SHIMIWI 2026 yanafanyika mkoani Kilimanjaro na yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 26 Septemba 2026. Mashindano hayo yataendelea hadi tarehe 7 Oktoba 2026 katika viwanja mbalimbali vya michezo vilivyopo mjini Moshi.