Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Nishati leo leo tarehe 24 Septemba imeibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya timu ya Bunge katika michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani Kilimanjaro.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fadhili Msigwa, amesema ushindi huo umeongeza morali kwa wachezaji na kueleza kuwa lengo la timu ni kufanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa wa SHIMIWI 2027.
Msigwa amesema katika mchezo wao wa awali uliochezwa tarehe 23, timu hiyo ilipoteza kwa mabao 3–2 dhidi ya Taasisi ya Umwagiliaji. Hata hivyo, amesema matokeo hayo yaliwapa nafasi ya kutathmini mapungufu na kujipanga zaidi kwa ajili ya mchezo uliofuata.
Amesema nidhamu, juhudi na kujituma kwa wachezaji ni miongoni mwa mambo yanayowapa matumaini ya kufanya vizuri katika michuano hiyo na kufikia malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wa timu ya wanawake ya mpira wa pete, jana iliibuka na ushindi wa mabao 28–20 dhidi ya RAS Mara.
Katika mchezo wa leo, timu hiyo ya Pete ya Wanawake imetoka sare ya mabao 25–25 dhidi ya wapinzani wao Timu ya Mashitaka.
Matokeo hayo yanaendelea kuonyesha ushindani wa timu ya Wizara ya Nishati katika michezo mbalimbali inayoshiriki kwenye michuano ya SHIMIWI mwaka huu.
Akizungumzia ushiriki wa timu hiyo, Msigwa amewashukuru Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati kwa kuwawezesha watumishi kushiriki michuano hiyo na kuipa nafasi Wizara ya Nishati kupeperusha bendera yake katika michezo inayoendelea mkoani Kilimanjaro.
Mbali na mpira wa miguu na mpira wa pete, Wizara ya Nishati inashiriki pia katika michezo mbalimbali ikiwemo baiskeli, drafti, darts, riadha, karata na bao.

