Serikali mkoani Morogoro imeanza utekelezaji wa hatua za kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji, huku ikitoa muda wa siku 60 kuhakikisha changamoto hiyo inapata ufumbuzi wa kudumu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Cuthbert Sendiga, amesema serikali imejipanga kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika, sambamba na kuchukua hatua dhidi ya viongozi watakaobainika kuchochea au kuendeleza migogoro hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika kipindi hicho cha siku 60 serikali itafanya kazi ya kutambua maeneo yenye migogoro, kusikiliza pande zote zinazohusika na kuhakikisha maamuzi yanayolenga kuleta amani na usalama yanatekelezwa.
Amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi watakaobainika kutumia nafasi zao kuchochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha amani na kuvuruga shughuli za uzalishaji.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa sahihi na kufuata taratibu zilizowekwa katika utatuzi wa migogoro, badala ya kuchukua sheria mkononi.
