NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGENI rasmi katika mahafali ya Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Mkombozi, Kata ya Mkimbizi, Manispaa ya Iringa, Ezra Msiliova, ameanzisha zoezi la kumchangia mwalimu wa kujitolea shuleni hapo, Khalid Nyangatuke, akimtaja kuwa ni miongoni mwa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya shule hiyo.
Msiliova, ambaye pia ni mfanyabiashara na mkandarasi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mahafali hayo yaliyowakutanisha wanafunzi, wazazi, walimu na viongozi wa shule.
Alisema ameguswa na mchango wa Nyangatuke katika kuwalea na kuwafundisha wanafunzi, akieleza kuwa utendaji wake umemfanya kuwa mwalimu anayependwa na wanafunzi pamoja na wazazi.
“Ni kidogo lakini naamini kitaweza kumsaidia kufanya vizuri zaidi. Tufanye kitu kwa ajili yake kwa sababu amekuwa akifanya kazi kubwa hapa,” alisema Msiliova.
Aidha, Msiliova alitoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo kwa kumchangia mwalimu huyo, huku akisisitiza kuwa mchango wa mtu unaweza kuwa mdogo kwa thamani lakini ukawa na maana kubwa kwa anayepokea.
Msiliova alisema uamuzi wake wa kuisaidia shule hiyo umetokana pia na historia yake ya kufanya shughuli mbalimbali katika Kata ya Mkimbizi, hivyo kuona umuhimu wa kurejesha sehemu ya kile alichopata kwa jamii.
Pia Msiliova aliahidi kuchangia uwekaji wa umeme katika darasa moja la Shule ya Msingi Mkombozi, akisema atatumia taaluma yake ya ujenzi kuhakikisha kazi hiyo inafanyika.
Msiliova pia alisema angependa darasa hilo lifanyiwe maboresho kwa namna ambayo litakuwa mfano kwa madarasa mengine na kuonyesha mchango wa wadau katika kuboresha mazingira ya elimu.
Akizungumza na wanafunzi waliohitimu Darasa la Saba, Msiliova aliwataka kutokukimbilia mambo mengine badala yake waweke mkazo katika masomo wanapoingia sekondari.
Aliwataka wanafunzi hao kuendelea kujituma, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa kutimiza ndoto zao na kufikia mafanikio katika maisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shule ya Msingi Mkombozi, Gerald Malekela, aliwashukuru walimu kwa kazi wanayoifanya na kusema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma licha ya changamoto mbalimbali za miundombinu.
Malekela pia aliwataka wazazi kutokubadili shule za watoto wao kwa msukumo wa kuona kwamba shule binafsi pekee ndizo zenye uwezo wa kutoa elimu bora.
Alisema walimu wa Mkombozi wamewajengea wanafunzi msingi mzuri wa kuendelea na elimu ya sekondari na kuwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi na elimu ya watoto wao.
“Tusifanye maamuzi kwa mihemko. Kama uwezo wako unaruhusu mtoto kusoma shule ya serikali, muache mtoto asome. Cha muhimu ni kumsimamia na kushirikiana na walimu,” alisema.
Mwenyekiti huyo pia aliomba wadau mbalimbali kuendelea kuisaidia shule hiyo katika kukabiliana na changamoto za miundombinu, akisema pamoja na kufanya vizuri kitaaluma, bado shule inakabiliwa na mahitaji mbalimbali.
Kwa upande wake, mwalimu wa kujitolea, Khalid Nyangatuke, alimshukuru Msiliova kwa utayari wake wa kumsaidia na kuahidi kuendelea kulitumikia eneo hilo kwa ajili ya wanafunzi.
Nyangatuke pia aliomba viongozi na wadau wengine kuangalia namna ya kumuunga mkono ili aweze kuendelea kufanya kazi katika shule hiyo, akisema amejenga uhusiano mzuri na wanafunzi, wazazi na jamii inayozunguka shule.