Na Ashrack Miraji, Same

Mkuu wa Wilaya Shikizi – Same, Mhe. Rukia Zuberi, amewasisitiza wanafunzi wa Mafunzo ya Awali ya Jeshi la Akiba, kundi la 30/2026/27, kuhakikisha wanazingatia mafunzo hayo ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya katika maisha yao, jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe. Rukia alitoa wito huo Leo tarehe 17/9/2026 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Awali ya Jeshi la Akiba (Mgambo), kundi la 30/2026/27, yanayofanyika katika Kata ya Vumari wilayani Same, yenye jumla ya wanafunzi 40 kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Rukia amewataka wanafunzi hao kuwa na bidii katika mafunzo, kuzingatia nidhamu, kuwa na uvumilivu na ustahimilivu, pamoja na kuhakikisha wanalinda afya zao wakati wote wa mafunzo na baada ya mafunzo.

Kwa upande wake, Mshauri wa Jeshi la Akiba amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania ili waweze kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya nchi, anga na maeneo ya baharini, pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwa wazalendo, wenye nidhamu na utayari.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rukia amewasisitiza wananchi wote wa Wilaya ya Same kuendelea kuchukua tahadhari mapema kutokana na matarajio ya mvua kubwa za El NiƱo, ikiwemo kuhama kwa wakati kutoka maeneo hatarishi, kuhifadhi chakula na mahitaji muhimu, pamoja na kuhakikisha njia za maji na mitaro zinakuwa safi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.