Kamati ya Makatibu Wakuu na Wataalamu kutoka Wizara na Taasisi za Serikali imehimizwa kuandaa mwelekeo wa kisera na kitaasisi ili kuhakikisha msimamo wa Tanzania unaakisi vipaumbele vya kitaifa kuelekea Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama Zinazotekeleza Mkataba wa Nairobi (COP 12).
Hayo yamesemwa Septemba 16, 2026, Unguja Zanzibar na Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu na Watalaam kilichojadili maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa COP 12.
Waziri Hamza amesema dhamana iliyokabidhiwa Tanzania kuelekea mkutano huo ni heshima kubwa kwa taifa hivyo, kunahitaji maandalizi madhubuti, mshikamano na uratibu wa karibu wa taasisi zote za kisekta.
“Mkutano huu una umuhimu mkubwa katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambazo zinatilia mkazo maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho” amesema Hamza.
Aidha Hamza amesema Kamati hiyo inapaswa kuweka msisitizo katika maeneo sita ya kimkakati ambayo ni uimarishaji uchumi wa buluu unaozingatia uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali, kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii za pwani.
Amebainisha masuala mengine ni pamoja na kuimarisha hatua za kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa bahari, kulinda mifumo ya ikolojia muhimu ikiwemo mikoko, matumbawe na maeneo ya pwani.
Amesema msisitizo huo unatokana na ukweli kuwa rasilimali za bahari zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali, utupaji wa taka bahari na hivyo kuhitajika kuwepo wa sauti ya pamoja kulinda rasilimali hizo.
Ameeleza kuwa mwelekeo m adhubuti kuelekea mkutano huo kutawezesha kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uongozi wa uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani katika ukanda wa Magharibi ya Bahari ya Hindi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amesema Kamati ya Makatibu imejipanga vyema katika kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa kuelekea Mkutano wa COP 12.
”Tumepanga kuhakikisha Watanzania wote wanapata faida kupitia mkutano wa COP 12 utakofanyika Tanzania….ushauri, maoni na mapendekezo yaliyotolewa na watalaamu yatachakatwa na kujadiliwa kwa kina zaidi” amesema Dkt. Muyungi.
Mkataba wa Nairobi kuhusu Usimamizi na Uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi ya Bahari ya Hindi unatekelezwa na Nchi Wanachama 10 ambazo ni Tanzania, Komoro, Kenya, Somalia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli na Ufaransa.

