Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umetakiwa kubadili fikra na kujiendesha kibiashara ili kuwa mfano wa kuigwa na makampuni ya uzalishaji wa mbegu nchini.
Amesema Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) wakati akizindua kikao kazi cha siku mbili cha Meneiimenti ya ASA na Wasimamizi wa Mashamba tarehe 16 Septemba 2026, katika hoteli ya Vizano, jijini Dodoma.
“Kilimo ni sayansi. Ni lazima ASA iwe na mipango thabiti ya kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa wakulima kwa wakati,” amesisitiza Mhe. Silinde.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuongeza tija, kipato cha mkulima na kuhakikisha usalama wa chakula na lishe nchini, ambapo msingi wa mafanikio hayo ni upatikanaji wa mbegu bora.
Mhe. Silinde alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, ASA inatakiwa kushirikiana na Sekta Binafsi ili kufanikisha uzalishaji wa mbegu tani 105,000. Amesisitiza zaidi kuwa ASA kuongeza mazao ya Mafuta kutoka tani 2,246,000 hadi tani 2,300,000; kuongeza Ngano kutoka tani 115,826 hadi tani 200,000; na kuongeza mazao ya Bustani kutoka tani 9,781,236 hadi tani 10,000,000.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Mhandisi Innocent Masaka, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Menejimenti yake na na Wasimamizi wa Mashamba ili kuongeza ufanisi, uadilifu na uwajibikaji katika uzalishaji wa mbegu bora na mapato ya ASA. Amesisitiza kuwa utekelzaji wa DIRA 2050, Agenda 10/30 na Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo 2050 kama nguzo za kupata matokeo yenye tija katika tasnia ya mbegu.


