BANGKOK, Thailand:
Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuchukua nafasi muhimu katika kuunda kizazi kijacho cha uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia duniani, kwa kuendeleza rasilimali zake kwa viwango vya juu na kujenga mnyororo jumuishi wa thamani wa gesi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, wakati akishiriki mjadala wa kimataifa wenye mada “The New Energy Powers: Who Will Shape the Next Era of Gas Supply?” katika Mkutano wa Gastech 2026 unaofanyika Bangkok, Thailand.
Mjadala huo umeangazia mabadiliko yanayoendelea katika soko la gesi duniani, changamoto za kijiografia na kisiasa, mabadiliko ya mahitaji ya nishati, kuibuka kwa vyanzo vipya vya usambazaji wa gesi pamoja na namna nchi zenye rasilimali ya gesi zinavyoweza kujipanga kuwa miongoni mwa wazalishaji na wasambazaji muhimu kuelekea kizazi kipya.
Akizungumza katika mjadala huo, Mhe. Salome amesema uzoefu wa Tanzania umeonyesha kuwa na rasilimali kubwa ya gesi pekee hakutoshi, bali thamani ya rasilimali hiyo huonekana pale inapoweza kubadilishwa kuwa nishati ya uhakika, yenye ushindani na inayochochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema historia ya gesi nchini Tanzania, ikiwemo ugunduzi wa gesi katika Songo Songo katika miaka ya 1970 na kuanza kwa uzalishaji wa kibiashara mwaka 2004, inatoa fundisho kwamba ugunduzi wa rasilimali pekee hauleti thamani bila uwekezaji, miundombinu, sera rafiki kwa uwekezaji, soko linalokua na dhamira ya pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi.
Tanzania kwa sasa ina zaidi ya trilioni 57 za futi za ujazo za gesi asilia zilizogunduliwa, huku sehemu kubwa ya rasilimali hizo ikiwa katika maeneo ya bahari kuu.
Pamoja na rasilimali hizo kubwa, Tanzania imeendelea kutumia gesi ya nchi kavu na maji ya kina kifupi kama kichocheo cha maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa Mhe. Salome, Songo Songo na Mnazi Bay zimekuwa nguzo muhimu katika mfumo wa nishati wa Tanzania, zikichangia uzalishaji wa umeme na kuwezesha matumizi ya gesi katika viwanda, taasisi, kaya na sekta ya usafirishaji kupitia matumizi yanayokua ya gesi asilia iliyobanwa (CNG).
Kuunganisha Gesi na Soko la Dunia Mhe. Makamba amesema moja ya mafanikio muhimu ya Tanzania ni kuanza kuunganisha rasilimali za gesi na masoko ya Dunia, huku matumizi ya gesi yakipanuka kutoka katika uzalishaji wa umeme hadi viwanda, taasisi, kaya na sekta ya usafirishaji.
Amesema kwa sasa, matumizi ya gesi nchini katika uzalishaji wa umeme ni asilimia 69 huku asilimia 27 ikitumika viwandani, asilimia 3 katika usafirishaji na asilimia 1 katika taasisi na kaya.
Amesema mgawanyo huo unaonyesha kuwa Tanzania haitumii gesi kama rasilimali ya nishati pekee, bali pia kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda, kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha Mhe. Salome amesisitiza kuwa matumizi ya gesi katika soko la ndani na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuuza gesi nje ya nchi havipaswi kuonekana kama mikakati inayokinzana, bali kama sehemu ya mkakati mpana wa kukuza soko la gesi na kuongeza thamani ya rasilimali hiyo kwa Taifa.
Amesema masoko ya ndani na kikanda yanaweza kutoa manufaa ya kiuchumi kwa haraka, kujenga miundombinu na kuongeza uwezo wa ndani, wakati miradi mikubwa ya kuuza gesi katika masoko ya kimataifa inafungua fursa za uwekezaji mkubwa, teknolojia na upatikanaji wa masoko ya kimataifa.
Tanzania katika kizazi kipya cha gesi duniani
Akijibu swali la msingi la mjadala kuhusu nchi zitakazokuwa mstari wa mbele katika kizazi kipya cha usambazaji wa gesi duniani, Mhe. Makamba amesema si lazima ziwe nchi zenye rasilimali nyingi zaidi, bali zile zitakazokuwa na mikakati bora ya uwekezaji, miundombinu ya usambazaji, upatikanaji wa masoko ya kimataifa na ushirikishwaji mpana wa wananchi katika mnyororo wa thamani wa gesi.
Amesema Tanzania ina fursa ya kuwa miongoni mwa nchi hizo kutokana na ukubwa wa rasilimali zake, nafasi yake ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki, ongezeko la mahitaji ya nishati pamoja na juhudi zinazoendelea za kuendeleza miundombinu na masoko ya gesi.
Mhe. Makamba amesema Tanzania inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali ya gesi inatumika kuongeza usalama wa nishati nchini, kuchochea uwekezaji na viwanda, kuongeza ajira na mapato ya Taifa, huku ikiiwezesha nchi kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa gesi wa kikanda na kimataifa.
Amesema hatua hizo zinaifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kutumia rasilimali zake za gesi si kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya sasa pekee, bali pia kujenga msingi wa ushindani wa Taifa katika kizazi kijacho cha soko la gesi duniani.

