Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

CHAMA cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU) kimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na TIB Rasilimali Limited, ikiwa ni hatua ya kuimarisha elimu ya fedha, akiba, uwekezaji na ustawi wa kiuchumi kwa wanachama wake.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Septemba 14, 2026, Katibu Mkuu wa TAREWU, Dkt. Michael Marere, amesema ustawi wa mwanachama hauishii katika masuala ya maslahi ya kikazi pekee, bali unahitaji pia kuwa na maarifa sahihi ya fedha, uwezo wa kupanga na kusimamia kipato pamoja na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Amesema TAREWU imeweka elimu ya fedha na ustawi wa kiuchumi kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu katika Mpango Mkakati wake wa Pili wa mwaka 2026–2030, kwa lengo la kuwawezesha wanachama kukabiliana na changamoto za kiuchumi.

Dkt. Marere amesema Chama hicho kinataka kujenga utamaduni endelevu wa elimu ya fedha, ambapo wanachama watawezeshwa kuelewa fedha zao, kupanga matumizi, kujenga akiba, kuwekeza kwa uelewa na kufanya maamuzi yatakayolinda ustawi wao wa sasa na wa baadaye.

Amesema ushirikiano na TIB Rasilimali Limited ni hatua ya kimkakati itakayosaidia utekelezaji wa mpango huo kwa vitendo, huku elimu ya fedha ikitumika kama nyenzo ya kujenga ustahimilivu wa kifedha na kuboresha maisha ya wanachama pamoja na familia zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIB Rasilimali Limited, Brighton Ross Konemo, amesema makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha wanachama wa TAREWU kupata elimu, maarifa na fursa za kujenga ustawi wao wa kifedha kupitia masoko ya mitaji.

Konemo amesema mfanyakazi hapaswi kutegemea mshahara pekee, bali anapaswa kutumia kipato chake kama mwanzo wa kujenga akiba, kufanya uwekezaji na kumiliki mali kwa ajili ya maisha ya sasa na ya baadaye.

Amesema TIB Rasilimali Limited itafanya kazi kwa karibu na TAREWU kutoa elimu kuhusu uwekezaji katika hisa, hati fungani za Serikali na fursa nyingine zinazopatikana katika masoko ya mitaji, pamoja na kuwawezesha wanachama kupanga fedha zao na kuanza kuwekeza kulingana na uwezo wao.

Amesema lengo ni kuhakikisha mwanachama akiwa Dar es Salaam, Dodoma, Arusha au sehemu nyingine nchini anaweza kupata huduma za uwekezaji kwa urahisi kupitia mtandao, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwekezaji wa muda mrefu.

Konemo amesema mfanyakazi anayefanya kazi kwa miaka mingi anapaswa kujiuliza ni mali gani ameweza kujenga kutokana na kipato chake, ikiwa ni pamoja na kuwa na akiba, kumiliki hisa au kuwa na vyanzo vingine vya mapato vinavyotokana na uwekezaji.

Amesema maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuanza mapema, kwa kuwa pamoja na pensheni kuwa muhimu, mfanyakazi anapaswa kuwa na vyanzo vingine vya mapato kutokana na uwekezaji alioujenga akiwa kazini.

Amesema TIB Rasilimali Limited na TAREWU zinakusudia kutengeneza mfuko maalum kwa ajili ya wanachama, huku akisisitiza kuwa utiaji saini wa makubaliano hayo si mwisho wa mchakato, bali ni mwanzo wa utekelezaji wa ushirikiano huo.

Amesema mafanikio ya ushirikiano huo yatapimwa kwa idadi ya wanachama watakaopata elimu ya fedha, huduma za masoko ya mitaji na kuanza kufanya uwekezaji, akitaka wanachama kubadilika kutoka kuwa wapokeaji wa mishahara pekee na kuwa wawekezaji na wamiliki wa mali.

Konemo ameshukuru uongozi wa TAREWU kwa kuamini katika ushirikiano huo, akisema TIB Rasilimali Limited iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Chama hicho kuhakikisha makubaliano hayo yanazalisha matokeo halisi na kujenga msingi imara wa kifedha kwa wanachama.