Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Serbia, mwenye makazi yake Roma, Italia, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk, amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Belgrade tarehe 14 Septemba 2026.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Hati hizo, Balozi Mbarouk amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Rais Mhe. Aleksandar Vučić, Serikali na wananchi wa Serbia, na kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Balozi Mbarouk ameeleza vipaumbele vya kipindi chake cha uwakilishi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, hususan katika maeneo ya biashara, kilimo, uwekezaji na elimu. Aidha Mheshimiwa Mbarouk ameeleza dhamira ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Serbia na wadau mbalimbali katika kuendeleza maeneo hayo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Rais Vučić amempongeza Balozi Mbarouk kwa kuteuliwa kwake na kumtakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake ya kidiplomasia nchini Serbia, huku akiahidi kumpa ushirikiano katika kipindi chake cha uwakilishi.