Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

MRADI wa Digital Tanzania umewezesha kuboresha mawasiliano ya kimtandao na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa njia ya kielektroniki, huku Serikali ikieleza kuwa utekelezaji wake umeleta mafanikio katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu, mifumo ya kidijitali na ujenzi wa uwezo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 14,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Kiwango, amesema mradi huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa mawasiliano, hasa maeneo ya vijijini yaliyokuwa na changamoto ya huduma hiyo.

Amesema kupitia mradi huo, minara ya mawasiliano imejengwa katika maeneo mbalimbali ambayo awali hayakuwa na mawasiliano, huku teknolojia ikiboreshwa hadi kufikia 3G na 4G, hatua inayowawezesha wananchi kutumia intaneti na huduma mbalimbali za kidijitali.

Kwa mujibu wa Kiwango, mradi umewezesha pia taasisi za Serikali, ikiwemo mamlaka za Serikali za mitaa, kuunganishwa na mitandao ya kidijitali inayowawezesha watumishi kutumia mifumo ya Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema miongoni mwa mifumo iliyowezeshwa ni mfumo wa kupima utendaji wa watumishi wa umma, maarufu kama PEPMIS, unaotumika katika taasisi za umma, pamoja na mfumo wa Daftari la Huduma za Serikali unaompa mwananchi taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali.

Ameeleza kuwa mfumo huo unamwezesha mwananchi kufahamu huduma anayohitaji, mahali inapopatikana, nyaraka anazotakiwa kuwa nazo, muda wa kupata huduma na gharama husika, hivyo kupunguza usumbufu wa kufika katika ofisi za Serikali bila taarifa kamili.

Kiwango amesema mradi pia umewezesha kuunganishwa kwa mifumo mbalimbali ya Serikali ili iweze kubadilishana taarifa, hatua ambayo inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kupunguza ulazima wa mwananchi kutoa taarifa zilezile mara kwa mara katika taasisi tofauti.

Amesema zaidi ya vijana 500 wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika maeneo mbalimbali ya teknolojia ya kidijitali, ambapo baadhi walipata mafunzo ndani ya nchi na wengine walipata fursa hiyo katika nchi zinazobobea kwenye teknolojia hizo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania, Bakari Mwangugu, amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021 umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni ikolojia ya kidijitali, muunganisho wa kidijitali na ujenzi wa uwezo wa watumishi na wananchi katika matumizi ya teknolojia.

Mwangugu amesema katika kuboresha mifumo, mradi umechangia maboresho katika taasisi mbalimbali ikiwemo RITA kwenye mifumo ya vyeti vya kuzaliwa na vifo, huku NIDA ikifanyiwa maboresho ya mfumo wake wa usajili na matumizi ya namba ya utambulisho wa mwananchi katika huduma mbalimbali.

Amesema namba ya NIDA imepewa matumizi mapana kupitia dhana ya Jamii Namba, inayolenga kurahisisha utambulisho wa mwananchi anapopata huduma katika taasisi mbalimbali ikiwemo benki, TRA, Serikali na Uhamiaji.

Amesema tathmini ya mradi inayofanyika inalenga kupitia utekelezaji wa malengo yote yaliyowekwa tangu mwaka 2021, ikiwemo miundombinu na mifumo ya kidijitali pamoja na ujenzi wa uwezo, ili kubaini mafanikio yaliyopatikana na maeneo ambayo bado yanahitaji maboresho wakati mradi ukielekea ukingoni.