Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Japan zimedhamiria kuendelea kuimarisha na kupanua wigo wa ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yao, kwa kuendeleza maeneo yenye maslahi ya pamoja yatakayochochea maendeleo na kuleta manufaa kwa mataifa yote mawili.
Dhamira hiyo imeelezwa Septemba 14, 2026, jijini Dodoma wakati wa mazungumzo ya pande mbili kati ya Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Felista Rugambwa, na Bw. Horonori Suzuki, Mkurugenzi wa Kitengo cha Pili cha Afrika katika Idara ya Masuala ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilijadili namna ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya maendeleo, miundombinu, biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha mahusiano baina ya wananchi wa Tanzania na Japan.
Aidha, pande hizo zimethibitisha dhamira ya kuendelea kujenga na kuimarisha ushirikiano huo ili kuongeza manufaa ya pamoja, kukuza mahusiano ya kirafiki na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania.

