Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

USHIRIKIANO kati ya Serikali na sekta binafsi umetajwa kuwa chachu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuongeza fursa za wananchi kupata elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi, alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Shule ya Msingi Kibaha Independent Pre and Primary School (KIPS), akieleza kuwa sekta binafsi inaendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuendeleza elimu nchini.

Shilingi alieleza elimu ni ibada na kwamba wadau wanaoamua kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu wanafanya jambo muhimu kwa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa uwekezaji huo unaendana na juhudi za kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo kuinua ubora wa elimu.

Alitaja miongoni mwa wawekezaji hao kuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya Njuweni, Yusuf Mfinanga, ambaye amesema anawekeza katika shule tatu za msingi, ambazo ni KIPS, KIPS Annex na KIPS Msangani, pamoja na Njuweni Institute of Hotel Catering and Tourism Management na shule tatu za sekondari ambazo ni Vuchama Ugweno Islamic, Mangio na Pwani Sekondari.

Aidha, Shilingi alitoa wito kwa wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba kuendelea na masomo hadi elimu ya juu, akieleza kuwa ulimwengu wa sasa unahitaji wahitimu wenye elimu, maarifa na upeo mpana wa kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Kwa upande wake, Mfinanga alisema Pwani Sekondari inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2027, hatua ambayo itaongeza fursa za elimu ya sekondari kwa vijana wa Kibaha, Pwani na maeneo mengine.

Alisisitiza umuhimu wa wanafunzi na vijana kuwa na maadili mema, huku akiwataka wazazi kufuatilia mwenendo wa watoto wao na kuhakikisha wanalelewa katika misingi inayojenga tabia njema.

Mwalimu Mkuu Salim Nkumbilwa, alieleza jumla ya wanafunzi 179 wamehitimu Darasa la Saba kutoka shule tatu za KIPS, KIPS Annex na KIPS Msangani.

Nkumbilwa anasema KIPS ilianzishwa mwaka 2001 ikiwa na wanafunzi tisa, na kwamba katika kipindi cha miaka 25 imeendelea kukua, huku akiishukuru Serikali kwa maboresho ya mitaala ambayo amesema yamechangia shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma.