Benki ya NMB imeorodheshwa katika nafasi ya tisa duniani ndani ya Daraja la Sita la benki zenye mali ya kati ya Dola za Marekani bilioni 3 na bilioni 10. NMB ni miongoni mwa benki 500 kutoka nchi 89 zilizojumuishwa katika orodha ya Forbes ya World’s Top Performing Banks 2026.
Forbes na Statista zilifanya tathmini hiyo kwa kuzingatia uwezo wa kupata faida, ukuaji na ubora wa mapato, uimara wa mtaji na vyanzo vya fedha, pamoja na ubora wa mali na ufanisi wa uendeshaji. Mwaka 2025, NMB iliripoti faida baada ya kodi ya takribani Sh760 bilioni na mali ya Sh17.6 trilioni.
Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, amesema utambuzi huo unaakisi mageuzi ya muda mrefu ya benki na uwezo wa sekta ya benki Tanzania kushindana kimataifa.
Zaipuna amesema NMB itaendelea kutumia ukubwa wake, teknolojia, ushirikiano na uwezo wa kifedha kupanua upatikanaji wa mitaji katika kilimo, viwanda, biashara, miundombinu na uchumi wa kidijitali, ikiwa ni sehemu ya kusaidia utekelezaji wa Dira 2050.
