Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imewapa siku 30 wataalamu wenye malimbikizo ya ada kukamilisha malipo yao, ikionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watafutiwa usajili bila taarifa nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 14, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, CPSP. Godfred Mbanyi, amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wataalamu kukamilisha ada zao kabla ya Bodi kuanza ukaguzi katika ofisi za umma na binafsi mikoani baada ya kumalizika kwa siku hizo 30.
Amebainisha kuwa mtaalamu yeyote anayefanya kazi za Ununuzi na Ugavi bila kusajiliwa na Bodi anavunja sheria, akisisitiza kuwa usajili huo unahusu sekta ya umma na binafsi.
Amesema kila mtaalamu aliyesajiliwa anawajibika kulipa ada kwa mujibu wa sheria na kanuni za PSPTB, huku mtaalamu anayeshindwa kulipa ada kwa kipindi cha miezi 24 akitakiwa kufutiwa usajili na jina lake kuondolewa kwenye daftari la Bodi.
Pia ameongeza kuwa PSPTB imeanza kujenga mfumo mpya wa usajili na inataka wataalamu kukamilisha malimbikizo yao ili kuepuka kuingiza taarifa zenye madeni kwenye mfumo huo.
Aidha ,amesema Kuwa baada ya siku 30 timu mbalimbali zitafanya ukaguzi katika ofisi za umma na binafsi mikoani kwa ajili ya kubaini watakaokuwa hawajatekeleza agizo hilo.
Amesema mtu ambaye atafutiwa usajili hataruhusiwa kuendelea kufanya kazi za Ununuzi na Ugavi, na endapo ataendelea kufanya kazi hizo atakuwa anatenda kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 46(2) na 46(3) cha Sheria ya PSPTB.
Kwa upande wa ada, amesema usajili wa PSPTB umegawanyika katika ngazi nne ambazo ni Authorized, Approved, Graduate na Technician, huku ada za mwaka zikiwa ni Shilingi 120,000 kwa Authorized, Shilingi 100,000 kwa Approved na Shilingi 60,000 kwa Graduate na Technician.
Amebainisha kuwa mtaalamu asipolipa ndani ya mwaka wa fedha huongezewa adhabu ya asilimia 50 katika miezi sita ya kwanza baada ya mwaka wa fedha.
Amebainisha Kuwa kwa ngazi ya Authorized, PSPTB ina zaidi ya wataalamu 400 ambao kwa sasa hawana madeni ya ada, huku karibu wataalamu 6,000 wakiwa na malimbikizo ya ada.
Amesema kwa ujumla PSPTB imewahi kusajili zaidi ya wataalamu 12,000, huku wataalamu 47 wakiwa tayari wamefutiwa usajili kutokana na migogoro ya ada.
Ameongeza kuwa baadhi ya wataalamu huacha kulipa ada baada ya kubadilishiwa majukumu ya kazi, lakini kwa mujibu wa PSPTB, usajili huo ni hitaji la kisheria na pia hutumika katika hatua za kupandishwa madaraja katika taaluma ya Ununuzi na Ugavi

