‎Dodoma

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Dodoma imeanza kukagua miundombinu ya barabara, madaraja, makalavati na mitaro ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa za El Nino.

‎Ukaguzi huo umelenga kubaini mapema maeneo hatarishi, kuimarisha miundombinu na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuziba mtiririko wa maji hatua inayolenga kupunguza hatari ya mafuriko, uharibifu wa barabara na kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua hizo.

‎Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miundombinu hiyo, Meneja wa TARURA wilaya ya Dodoma Mhandisi Emmanuel Mfinanga amesema maandalizi hayo yameanza mapema kwa kutambua maeneo yenye viashiria vya hatari na kuchukua hatua kabla mvua kubwa hazijasababisha madhara.

‎”Tunaendelea kupita na kukagua miundombinu yetu, maeneo ambayo tunaona kuna viatarishi tumeanza kufanya maboresho ili kuzuia athari zisijitokeze na kazi hii imeanza na ni endelevu”, amesema Mhandisi Mfinanga.

‎Amesema maeneo ambayo wanaona yana viatarishi wameanza kufanya maboresho ikiwemo kufanya usafi kwenye maingililio ya madaraja, usafi kwenye matoleo (downstream) ambapo zoezi hilo wanafanya kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji, kata, mitaa na vijiji.

‎Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na TARURA kulinda miundombinu ya barabara hususani mitaro, madaraja na makalavati na kuwataka wananchi waepuke kutupa takataka kwenye maeneo hayo ili yaendelee kudumu kwa muda mrefu kwani ikiziba watapata mafuriko lakini miundombinu hiyo ikiwa safi maji yatatiririka na kupunguza adha ya mafuriko.

‎Pia ameeleza kuwa serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali katika wilaya ya Dodoma ili kukabiliana na changamoto ya mvua ikiwemo ujenzi wa barabara ya Ilazo-Mbuyuni mita 250 pamoja na ujenzi wa mifereji kilomita 1.5 na ujenzi wa madaraja matatu ya mawe likiwemo SGR (Chidachi Kusini), Ntyuka (2) yote yenye urefu wa mita 14.

TARURA imechukua hatua hiyo ikiwa ni namna ya kujipanga kufuatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa taarifa ya utabiri wa hali ya hewa ikionesha uwepo wa mvua kubwa za Elnino ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya barabara na zoezi hilo la ukaguzi wa miundombinu linafanyika nchi nzima.