Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MWENYEKITI wa chama cha Wafanyabiashara wa madini Mkoa wa Manyara, Mokia Ole Mrefu, amesema wadau wa madini wa eneo hilo wanamkaribisha Mkuu mpya wa Mkoa huo Martine Shigela wakiwa na matumaini makubwa kwenye uongozi wake.

Ole Mrefu akizungumza na waandishi wa habari amesema wafanyabiashara wa madini wa Manyara wana matarajio makubwa na ujio wa mkuu mpya wa Mkoa wa Manyara, Martine Shegela kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Queen Cuthbert Sendiga aliyehamishiwa Morogoro.

“Tukiamini kuwa uzoefu wake Mheshimiwa Shigela katika sekta ya madini Mkoani Geita utasaidia kuendeleza sekta hii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Manyara,” amesema Ole Mrefu.

“Nikijibu swali lako ndugu mwandishi kuhusu matarajio ya wafanyabiashara wa madini kufuatia mabadiliko ya uongozi wa Mkoa wa Manyara, mimi Mokia Ole Mrefu nasema tunatarajia Mheshimiwa Shegela kuendeleza mazuri yaliyoachwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Queen C. Sendiga,” amesema.

Amesema matarajio yao ni kwamba Shegela atakuja kuanzia na kuendeleza pale alipofikia Mkuu wa Mkoa aliyehamishiwa Morogoro, Queen Sendiga.

“Tunategemea kwamba kazi nzuri aliyofanya Geita, ikiwemo kuwawezesha vijana wengi kufikia mafanikio makubwa kiuchumi, ataendeleza juhudi hizo hapa Manyara. Tunatumaini anakuja kutengeneza mabilionea wengine wengi zaidi kupitia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini,” kwenye mkoa wetu wa Manyara,” amesema Ole Mrefu.

PONGEZI ZETU ZA DHATI KWA MHESHIMIWA RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN

Amesema wanampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kufanya mabadiliko ya kiuongozi yenye lengo la kuimarisha utendaji wa Serikali.

“CHAMMATA Manyara tunamkaribisha rasmi mheshimiwa Martine Shegela Mkoani Manyara na kumhakikishia kuwa wafanyabiashara wa madini wako tayari kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake,” amesema.

SHUKRANI KWA MHESHIMIWA QUEEN SENDIGA

“Kwake Mheshimiwa Queen Sendiga tunamshukuru kwa kila hali. Alitulea vyema, alitupa ushirikiano wa kutosha na alisimamia mambo mengi kwa moyo wa kujitolea. Tunamshukuru sana kwa yote aliyoyafanya kwa Mkoa wa Manyara na hususan kwa wafanyabiashara wa madini Mkoa wa Manyara'” amesema Ole Mrefu