Mahakama ya Wilaya ya Mbulu imewahukumu aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamusta, Daniel Gidambisye Murayda, pamoja na Mhasibu wa shule hiyo, James Cosmas Bazil, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka yanayohusisha ukiukaji wa taratibu za manunuzi ya umma.
Hukumu hiyo imetolewa Septemba 10, 2026, na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Mbulu, Vitus Kapugi, katika shauri la uhujumu uchumi namba 14623/2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU, washtakiwa walikiuka kanuni za manunuzi ya umma wakati wa utekelezaji wa Water Sanitization Project katika Shule ya Msingi Nyamusta, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu.
Inadaiwa kuwa washtakiwa walishindwa kushindanisha wazabuni na kutoa zabuni ya kusambaza vifaa vya mradi vyenye thamani ya Shilingi 26,447,217.10, kwa upendeleo na kinyume na Sheria, Kanuni za Manunuzi ya Umma pamoja na miongozo ya utekelezaji wa miradi kwa mfumo wa Force Account.
Baada ya kusikilizwa kwa shauri hilo, Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote wawili na kuwahukumu kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani au kulipa faini ya Shilingi milioni moja.
Shauri hilo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Amiri Addy.
