Na Mwandishi wetu, Mirerani
KATIBU wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, Rachel Njau amewataka wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani kuwajali wafanyakazi wao kwa nyakati zote hata wakiugua.
Rachel Njau ameeleza hayo kwenye mkutano wa wachimbaji madini ya Tanzanite wa kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Ameewaasa wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuwa siyo vyema kuwajali na kuwapenda wachimbaji wao wakiwa wenye afya na kuwatelekeza washaugua.
Amesema baadhi ya wachimbaji wanafika ofisini kwake wanalalamikia wamiliki wa migodi wanawatelekeza pindi wakiugua siyo vyema.
Ameeleza kuwa hivi karibuni walitembelea hospitali ya Kibong’oto na kubaini baadhi ya wachimbaji wanaugua vifua ila wamiliki wa migodi hawasaidii chochote kwa matibabu.
“Wote tumezaa jamani tuwahudumie wafanyakazi wetu pindi wakiugua, tusiwapende wakiwa na afya pekee ya kufanya kazi,” amesema.
Mwenyekiti mstaafu wa MAREMA Sadiki Mneney amempongeza Rachel Njau kwa namna anavyofanya kazi ya ukatibu.
“Rachel ni mwanamke wa shoka anapaswa kupewa ushirikiano na wachimbaji wote kwani anajitoa mno na anatumia hata fedha zake kuendesha ofisi ya MAREMA,” amesema Mneney.
