Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya Kikao Kazi cha Kwanza cha Jukwaa la Ushauri la Wadau wa TRA kuhusu Maadili, kinachofanyika mkoani Morogoro, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na wadau katika kukuza maadili katika usimamizi wa kodi na forodha.

Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyowekwa wakati wa uzinduzi wa Jukwaa hilo tarehe 24 Aprili 2026, ambao ulikuwa mwanzo wa kujenga njia rasmi na endelevu ya kusikiliza maoni, changamoto na mapendekezo ya wadau kuhusu masuala ya maadili katika shughuli za TRA.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani wa TRA, Shaibu Mmari, amesema maadili si suala la ndani ya TRA pekee, bali ni msingi muhimu wa kujenga uhusiano wa kuaminiana kati ya Mamlaka, walipakodi na jamii kwa ujumla.

Amesema ni muhimu walipakodi kutendewa kwa heshima, maamuzi kutolewa kwa misingi ya sheria na taratibu zinazoeleweka, pamoja na huduma kutolewa kwa wakati na kwa usawa, hatua ambazo zinaongeza imani ya walipakodi na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari.

Aidha, Mmari amewataka wajumbe wa Jukwaa hilo kuzungumza kwa uwazi na kutoa maoni kuhusu maeneo ambayo yanaweza kuwa na changamoto za kimaadili, ikiwemo ucheleweshaji wa huduma, matumizi mabaya ya mamlaka, changamoto katika mifumo ya kidijitali na njia za kutoa taarifa, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa mapendekezo mahususi na yanayotekelezeka.

Kwa upande wake, Naibu Kadhi Mkuu, Sheikh Ali Khamis Ngeruko, amesema ni vyema watumishi wa TRA pamoja na walipakodi kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha kodi zinalipwa kwa haki na kwa hiari. Aidha, amewataka watumishi na walipakodi kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuzingatia uadilifu katika shughuli za kodi.

Kikao hicho kimewakutanisha wawakilishi kutoka vyama vya wafanyabiashara, walipakodi, washauri wa kodi, mawakala wa forodha, taasisi za Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini pamoja na viongozi na watendaji wa TRA, ambapo pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya maadili, kikao hicho kinajadili pia rasimu ya Hadidu za Rejea za Jukwaa zitakazoweka msingi wa utekelezaji wa majukumu yake na ushirikiano endelevu na wadau.