Na Shaban Juma, WAF – Arusha
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesisitiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru kuongeza kasi katika utoaji wa huduma bora za afya ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Dkt. Samizi ametoa msisitizo huo leo Septemba 09, 2026 jijini Arusha wakati akikagua utoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata huduma za afya, ambapo tayari imewalipia zaidi ya kaya 200,000 kiasi cha Shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kuwawezesha kupata huduma za matibabu kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote umeanza, ambapo kwa sasa Serikali imeanza na kaya maskini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wenye uhitaji wanapata huduma za afya bila kukabiliwa na changamoto ya gharama za matibabu.
Dkt. Samizi amewataka watendaji wa Hospitali ya Mount Meru kuhakikisha uwekezaji huo wa Serikali katika bima ya afya unaenda sambamba na utoaji wa huduma bora, za haraka na zenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha mfumo wa afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

