Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha VETA Mkoa wa Mbeya ikishirikiana na Jeshi la Magereza mkoani Mbeya imeanza mchakato wa kutambua, kutathmini na kurasimisha ujuzi wa ufundi stadi kwa wafungwa 100 walioupata wakati wakitumikia vifungo.

Mchakato huo ulioanza tarehe 27 Agosti 2026 unafanywa kwa ushirikiano na Chuo cha Ufundi cha Jeshi la Magereza Ruanda, jijini Mbeya, na unatarajiwa kukamilika Septemba 15, 2026.

Akizungumza kuhusu mchakato huo, Meneja wa Kanda ya Kusini Magharibi, Shomari Chololo waombaji waliojitokeza ni wamegawanyika katika stadi Ufundi Umeme (8), Ufundi Bomba (10), Ufundi Seremala (15), Ufundi Uashi (41), Uungaji na Uundaji Vyuma (12), Ushonaji (11), Huduma za Ndani na Usafi pamoja na Utengenezaji wa Sabuni (3).

Kupitia mchakato huo, wafungwa watakaokidhi vigezo wanatarajiwa kupata vyeti vinavyothibitisha ujuzi wao, hatua inayolenga kuwawezesha kutumia ujuzi huo kwa tija, ikiwemo kujiajiri, kuajiriwa au kuanzisha shughuli za uzalishaji baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao

Mchakato huo ni sehemu ya jitihada za kutambua na kuthibitisha ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo na uzoefu wa vitendo, ili wahusika waweze kuwa na uthibitisho rasmi wa uwezo wao wa kiufundi na kuutumia katika maisha yao baada ya kumaliza vifungo.

VETA huendesha programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL) ambapo mafundi hufanyiwa tathmini ya ujuzi wao, kubaini upungufu walio nao katika stadi husika, kisha kuandaliwa mafunzo ya muda mfupi kuziba upungufu na hatimaye kutunukiwa vyeti vya urasimishaji ujuzi.