Na mwandishi wetu, Mirerani 

WACHIMBAJI madini wa Mkoa wa Manyara, wametakiwa kuchukua tahadhari wakiwa wanafanya kazi ya kuchimba ili kukabiliana na mvua kubwa za El Nino pindi zikianza.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mji mdogo wa Mirerani.

Elisha amesema wachimbaji madini wanapaswa kuchimba kwa tahadhari, baada ya mamlaka ya hali ya hewa nchini kutangaza kuwa kutakuwa na mvua kubwa za El Nino.

Amesema wachimbaji wana jukumu la kujiandaa baada ya kutolewa taarifa kuwa kuna mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Novemba.

“Mwaka 1998 na mwaka 2008 kwenye machimbo ya Tanzanite tulipata maafa ya watu kufa kutokana na mvua hizo hivyo tuchukue tahadhari ili matukio hayo yasijirudie upya,” amesema Elisha.

Amesema wachimbaji madini wa mkoa huo wakibaini kuwa mvua zinanyesha maeneo yao wanapaswa kutoka ndani ya migodi ili kuepuka madhara yasitokee.

Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzanite na Makamu Mwenyekiti wa MAREMA, Money Yusuf amesema wachimbaji ambao hawajajengea migodi yao wafanye hivyo ili kuepuka ajali pindi mvua zikinyesha.

“Tunapaswa kujipanga na El Nino kwenye migodi yetu kwa kusafisha mitaro na kule kwenye mitobozano tuandae viroba na mabomba ya hewa,” amesema Money.

Mwakilishi wa Afisa Mlmadini mkazi (RMO) Paulo Msandae amesema wameendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na kuchukua tahadhari pindi mvua zikinyesha.

Mchimbaji mwingine Zephaniah Mungaya amesema ofisi ya RMO ilishatoa onyo la kuwepo vifusi vya mchanga hivyo migodi yenye vifusi iliandikiwa barua waondoe.