Mbarali, Mbeya – Wajawazito wanaopata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali wanatarajiwa kunufaika na vifaa tiba na vifaa vya kujifungulia vilivyotolewa na Yas Tanzania kupitia Kampeni ya Tumaini.

Msaada huo unalenga kuongeza upatikanaji wa vifaa muhimu na kusaidia hospitali hiyo kutoa huduma bora na salama zaidi kwa mama na mtoto.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Yas – Nyanda za Juu Kusini, Bw. Frank Protas Antony, alisema Kampeni ya Tumaini ni sehemu ya jitihada za Yas kusaidia jamii katika maeneo yenye uhitaji.

“Tunataka msaada huu uwe na matokeo ya moja kwa moja kwa wajawazito wanaofika hapa kupata huduma. Kampeni ya Tumaini itaendelea kufikia maeneo mengine nchini,” alisema Antony.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Dk. Yakub Sanga, aliipongeza Yas kwa msaada huo, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha huduma kwa wajawazito wanaohudumiwa hospitalini hapo.

Kwa upande wao, Muuguzi Mkuu Bi. Iman Mwakipusa na Kaimu Mganga Mfawidhi Dk. Albert Sichone walisema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza baadhi ya mahitaji ya vifaa muhimu vya uzazi hospitalini hapo.

Kampeni ya Tumaini inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kusaidia kuboresha mazingira ya huduma kwa wajawazito na kina mama wanaojifungua.