ADDIS ABABA, ETHIOPIA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.), ameshiriki na kuzungumza katika Mkutano wa Kanda ya Afrika wa Mapitio ya Nusu Muhula ya Mpango Kazi wa Doha (Doha Programme of Action), uliofanyika Septemba 8 na 9, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri na Maafisa waandamizi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, pamoja na wadau kutoka Sekta Binafsi, kwa lengo la kufanya tathmini ya nusu muhula ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Doha.
Aidha, mkutano huo umejadili changamoto za kimaendeleo zinazoikabili nchi zinazoendelea, hususan nchi zilizo katika kundi la nchi maskini zaidi duniani (Least Developed Countries – LDCs), pamoja na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuwezesha nchi hizo kujikwamua kiuchumi na hatimaye kutoka katika kundi hilo na kufikia hadhi ya nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.
Dkt. Maghembe ameshiriki katika mkutano huo akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).
Katika hotuba yake, Dkt. Maghembe ameelezea mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mipango ya maendeleo, ikiwemo juhudi za kuimarisha uchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza fursa za ajira na kukuza biashara, pamoja na kuimarisha huduma za kijamii.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali zinazolenga kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku ikishirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wa malengo ya maendeleo.
Dkt. Maghembe pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuziwezesha nchi zinazoendelea kukabiliana na changamoto za maendeleo, ikiwemo upatikanaji wa fedha, teknolojia, ujuzi na masoko, ili ziweze kujenga uchumi imara na endelevu.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kufuatilia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Doha na kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuziwezesha nchi zilizo katika kundi la LDCs kuimarisha uwezo wao wa kiuchumi, kujenga ustahimilivu na hatimaye kutoka katika kundi hilo.

