Na OWM – TAMISEMI, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametambuliwa kuwa kinara katika kuimarisha huduma za afya ya msingi kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini, hususan katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Aya ya Msingi (IPHC) kwa niaba ya Rais Samia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini Arusha (AICC), Septemba 9, 2026, Waziri Mkuu amesema mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kutambulika kimataifa, ikiwemo Rais Samia kutunukiwa Goalkeeper Award mwaka 2025 na kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika wa huduma za afya ya mama na mtoto mwaka 2026.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya, na sasa Serikali inaelekeza nguvu zaidi katika kuboresha ubora na ufanisi wa huduma hizo,” amesema Waziri Mkuu. Ameeleza kuwa vifo vitokanavyo na uzazi duniani vimepungua kutoka takribani 328 hadi 197 kwa kila vizazi hai 100,000 kati ya mwaka 2000 na 2023, hali inayoonesha kuwa malengo ya afya yanaweza kufikiwa kwa kuongeza uwekezaji na kutekeleza mipango madhubuti.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuongeza miundombinu, wataalamu na rasilimali nyingine muhimu, huku zaidi ya watumishi 16,000 wa sekta hiyo wakiajiriwa kati ya Desemba 2025 na mwaka 2026. Aidha, Serikali imejenga nyumba zaidi ya 430 za watumishi wa afya na inapanga kujenga takribani nyumba nyingine 2,000 kuelekea mwaka 2030. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote utawezesha wananchi, wakiwemo wenye kipato duni, kupata huduma bora kwa gharama nafuu na bila ubaguzi wa kipato.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema kati ya mahudhurio milioni 32.3 ya wagonjwa wa nje yaliyorekodiwa katika vituo vya afya vya umma, mahudhurio milioni 27.8, sawa na asilimia 86, yalikuwa katika vituo vya afya ya msingi. Aidha, kati ya vituo 8,288 vya afya vya Serikali nchini, vituo 7,946, sawa na asilimia 95.8, ni vya ngazi ya afya ya msingi vinavyomilikiwa na halmashauri. Ameongeza kuwa asilimia 96.6 ya vituo hivyo vimeunganishwa na mfumo wa GoTHOMIS na asilimia 87.6 vimeunganishwa na GePG, hatua inayoongeza ufanisi, uwazi na usimamizi wa mapato na huduma.
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla, amesema Mkoa huo umepokea zaidi ya Sh bilioni 94 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya msingi. Uwekezaji huo umechangia kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 382 hadi 450, kuajiriwa kwa watumishi wapya 823 wa kada za afya na kupatikana kwa magari 27 ya kuhudumia wananchi, hatua zilizosaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Akizungumza kwa niaba ya asasi za kiraia zinazoshughulikia masuala ya afya nchini, Bw. Amson Mwendamake amependekeza kuimarishwa kwa ushiriki wa jamii katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia mipango na bajeti za afya ya msingi. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufadhili wa ndani, kuwalinda wananchi walio katika mazingira hatarishi dhidi ya gharama kubwa za matibabu na kuimarisha uwajibikaji pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na wadau.
Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Afya ya Msingi unafanyika jijini Arusha kuanzia Septemba 9 hadi 11, 2026, ukiwakutanisha wataalamu wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya kujadili na kutathmini masuala ya afya ya msingi. Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote: Kuimarisha ugharamiaji endelevu wa huduma za afya, ufanisi na uboreshaji wa huduma katika ngazi ya msingi.”
