DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) imefanikiwa kunasa shehena mbili kubwa za dawa na vifaa tiba zisizosajiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3, zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 360.
Shehena ya kwanza yenye thamani ya Shilingi milioni 310 ilikamatwa Septemba 7, 2026, ikiwa na mabegi 20 yaliyotoka India na kubeba dawa mbalimbali ambazo hazikuwa na usajili wala vibali vya TMDA.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo amesema shehena hiyo ilibainika wakati wakaguzi wa Mamlaka hiyo wakifanya ukaguzi wa kawaida kupitia mfumo wa udhibiti wa mizigo.
“Wakaguzi wetu wamefanikiwa kukamata mabegi 20 yaliyokuja kutoka India. Yalikuwa na dawa nyingi sana zenye thamani ya Shilingi milioni 310. Hapakuwa na nguo wala vyakula. Tatizo kubwa ni kwamba dawa hizo zote hazikuwa na usajili wala vibali vyovyote vya TMDA,” amesema Dkt. Fimbo.
Amesema Septemba 9, 2026, TMDA imefanikiwa kunasa shehena nyingine yenye thamani ya Shilingi milioni 50, iliyokuwa na dawa na vifaa tiba mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dkt. Fimbo, shehena hiyo ilikuwa na sindano za lignocaine, bupivacaine, adrenaline na vitamini, pamoja na dawa zinazotumika kutibu magonjwa ya saratani, kifafa, shinikizo la damu na kisukari.
Amesema pia shehena hiyo ilikuwa na dawa aina ya OZEMPIC na GLP-1, ambazo zimekuwa maarufu mitandaoni kwa matumizi ya kupunguza uzito, pamoja na vifaa tiba vinavyotumika katika huduma za meno.
Dkt. Fimbo amesema dawa zisizosajiliwa ni hatari kwa afya ya wananchi kwa kuwa ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa na TMDA, hivyo matumizi yake yanaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupona, usugu wa dawa, ulemavu na hata vifo.
Amesema hadi sasa watu watano wamekamatwa na vyombo vya usalama na uchunguzi unaendelea ili kubaini zaidi kuhusu mtandao wa uingizaji wa dawa hizo nchini.
Dkt. Fimbo amesema dawa zote zilizokamatwa zitateketezwa baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na kisheria.
Aidha, TMDA imetoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini, ikisisitiza kuwa ni marufuku kuingiza bidhaa hizo bila kupata vibali husika.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wote watakaobainika kuhusika na uingizaji au usambazaji wa dawa na vifaa tiba visivyosajiliwa nchini.

