Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, hivyo kuna fursa kubwa kwa wawekezaji kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.

 Amesema Serikali inakaribisha wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, kiteknolojia na kitaalamu ili kushirikiana katika kufikia lengo hilo.

Mhe.Salome ameyasema hayo leo jijini Dodoma, katika Mji wa Serikali Mtumba, wakati alipofanya mazungumzo na watendaji kutoka kampuni ya PowerChina, wakiongozwa na Makamu wa Rais anayesimamia Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Yu Haian, waliofika Wizara ya Nishati kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya nishati nchini.

“Serikali inalenga kufikia ongezeko hili la uzalishaji kwa kutumia mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali vya nishati, ikiwemo maji, jua, upepo na jotoardhi, hatua itakayosaidia kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme vitakavyoimarisha usalama wa nishati na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.” Amesema Mhe. Salome

. Amesisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati nchini.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa PowerChina anayesimamia Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Yu Haian, amesema kampuni hiyo imevutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, hususan katika maeneo ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na uhifadhi wa umeme.

Bw. Yu amesema Tanzania ina rasilimali kubwa za maji, jua, upepo na jotoardhi ambazo zinaweza kutumika kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha usalama wa nishati.

 Ameeleza kuwa PowerChina imefanya utafiti kuhusu mipango ya Tanzania katika sekta hiyo na kuona fursa kubwa za ushirikiano na Serikali.

Ameongeza kuwa PowerChina ina uzoefu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati duniani, ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji, jua, upepo na jotoardhi, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa za kuhifadhi nishati.

Vilevile, Bw. Yu amesema PowerChina iko tayari kushirikiana na Serikali katika miradi ya nishati jadidifu, ikiwemo nishati ya jua, upepo na jotoardhi, pamoja na mifumo ya kuhifadhi umeme kwa kutumia betri na teknolojia ya pumped storage, ambayo inaweza kusaidia kuimarisha uthabiti wa gridi ya taifa