Na John Walter -Babati 
Kiwanda cha sukari cha Manyara Sugar, chini ya uongozi wa Meneja wake Kamlesh Mandan Khunti, kimeendelea kusogeza fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia mpango wa kuwawezesha kulima miwa kwa ajili ya kupata soko la uhakika.
Mpango huo umeanza kuwanufaisha wakazi wa Kata ya Bonga, ambapo wakulima watapatiwa mbegu za miwa, utaalamu wa kilimo pamoja na uhakika wa soko la mazao yao katika kiwanda cha Manyara Sugar kilichopo Kata ya Magugu.
Mbali na huduma hizo, wakulima watasaidiwa pia katika maandalizi na ulimaji wa mashamba yao, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana na uwepo wa kiwanda hicho.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Emmanuel Khambay, amepongeza juhudi hizo, akisema zinafungua fursa kubwa kwa wananchi kujikwamua kiuchumi.
Khambay amesema mpango huo unatarajiwa kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Babati, hususan maeneo yenye uhakika wa maji, ikiwemo maeneo yaliyopo pembezoni mwa Ziwa Babati, ambayo yana mazingira mazuri kwa kilimo cha miwa.
Amesema kilimo cha miwa kupitia mpango huo kitasaidia kuongeza ajira, kuongeza kipato cha kaya na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Babati, kutokana na uwepo wa soko la uhakika kupitia kiwanda cha Manyara Sugar.
Kwa upande wao, wakulima waliopokea fursa hiyo wameeleza furaha yao na kuahidi kuitumia ipasavyo, wakiamini kuwa kilimo cha miwa kitakuwa chanzo muhimu cha kipato na kuwawezesha kuboresha maisha yao.
Mpango huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuunganisha wananchi na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji wa viwanda katika Mkoa wa Manyara.