Happy Lazaro,Arusha .

Arusha. Tanzania Bikers Federation (TBF) imewataka waendesha pikipiki kubwa na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha kubwa la waendesha pikipiki kubwa litakalofanyika jijini Arusha katika eneo la Masai Camp, Oktoba 16 hadi 18 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arushs Katibu Mkuu wa Tanzania Bikers Federation, Emmanuel Bugabu, amesema tamasha hilo linalenga kuwakutanisha waendesha pikipiki kubwa kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuimarisha umoja wao, huku likitumia pia pikipiki kama chombo cha kuelimisha jamii kuhusu usalama barabarani. 

Bugabu amesema TBF ni mwavuli unaosimamia maslahi ya waendesha pikipiki kubwa, hususan wenye pikipiki zenye ujazo wa injini kuanzia CC 250 na kuendelea, na kuwa tamasha hilo litakuwa moja ya matukio makubwa ya kuunganisha utamaduni wa waendesha pikipiki bila kulenga mashindano. 

Amesema kila mkoa nchini una vilabu vya waendesha pikipiki, ikiwemo Northern Riders na Rock City kutoka Mwanza, Northern Bikers kutoka Arusha, pamoja na Ride With Us, vilabu vya chopper na vingine kutoka Dar es Salaam, hivyo tamasha hilo litatoa fursa ya kuwakutanisha pamoja na kujenga umoja.

“Waendesha pikipiki kubwa wamekuwa wakivutiwa na safari za umbali mrefu, hivyo wamechagua Arusha kutokana na nafasi yake kama moja ya vituo muhimu vya utalii nchini Tanzania.”amesema Bugabu.

“Mbali na burudani na kuonyesha utamaduni wa waendesha pikipiki, tamasha hilo litakuwa na shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo upandaji miti, uchangiaji wa damu na uhamasishaji kuhusu afya ya akili, kwa lengo la kutoa mchango chanya kwa jamii.”amesema Bugabu.

Bugabu ameongeza kuwa, tamasha hilo linatarajiwa kushirikisha waendesha pikipiki wenye pikipiki kuanzia CC 250 na kuendelea, huku waandaaji wakilenga pia kupata ushiriki mkubwa wa wananchi na wageni kutoka maeneo mbalimbali

Aidha, Bugabu amefafanua kuwa, waandaaji wamepata wadhamini mbalimbali ambao wameunga mkono tamasha hilo, na kwamba majina yao pamoja na taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitatolewa kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya Tanzania Bikers Federation.

Aidha amewataka wakazi wa mkoa wa Arusha na wananchi kutoka maeneo mengine nchini kujitokeza kwa wingi na kusema waandaaji wameandaa burudani na shughuli mbalimbali, ikiwemo ujio wa msanii siku ya Jumamosi.

“Tunawaomba wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi,tumeandaa vitu vizuri sana, kutakuwa na burudani na shughuli mbalimbali ambazo tunaamini zitawafurahisha,” amesema Bugabu.

Kaulimbiu ya TBF ni “Umoja wa Bikers – Tanzania na Afrika Mashariki,” huku tamasha likitarajiwa kushirikisha waendesha pikipiki kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.