Tahir Mussa, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade; Juma Burhan, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA; na Fatma Ahmed, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara, Benki ya Stanbic, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Zanzibar jana kutangaza ushirikiano huo.
……………
Stanbic Bank Tanzania (@stanbicbanktz) imetangaza udhamini wa TZS milioni 200 kwa maonesho ya Fahari ya Zanzibar 2026, hatua inayoonesha dhamira yake ya kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na kuwawezesha wafanyabiashara, wajasiriamali na jamii kwa ujumla.
Maonesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 14 Septemba 2026 katika Viwanja vya Maisara, Zanzibar, yakibeba kaulimbiu “Bidhaa Zetu Ndio Fahari Yetu.” Zaidi ya washiriki 300 na wageni 15,000 wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo, linalolenga kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Maonesho hayo yameandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Kama mdhamini mkuu, Stanbic Bank itatumia maonesho hayo kuonesha suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kusaidia ukuaji wa biashara, kuwezesha biashara za ndani na za kimataifa, pamoja na kukuza ushiriki wa wafanyabiashara katika fursa za masoko mapya.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa benki hiyo, Fatma Ahmed, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara, Stanbic Bank Tanzania, alisema ushirikiano huo unaakisi imani ya benki katika nafasi ya Zanzibar kama kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji.
“Fahari ya Zanzibar ni jukwaa linaloonesha ubunifu, juhudi na uwezo wa wafanyabiashara wa Zanzibar. Sisi tunaendelea kujenga mazingira yatakayowasaidia kukuza biashara zao, kuongeza ushindani na kufikia masoko mapana zaidi. Zanzibar ni nyumbani kwetu, na tutaendelea kuunga mkono safari yake ya maendeleo ya kiuchumi,” alisema.
Maonesho hayo pia yatahusisha mijadala na shughuli mbalimbali zinazolenga vijana, ubunifu, utalii, sanaa, biashara na ujumuishaji wa kiuchumi.
