Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wameanza vyema kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.

Mchezo huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika umechezwa leo, Septemba 6, 2026, katika Uwanja wa Taifa wa Bingu, Lilongwe, nchini Malawi.

Bao pekee la Simba limefungwa dakika ya 64 ya kipindi cha pili na Anicet Oura, akiiwezesha timu hiyo kurejea Tanzania ikiwa na mtaji wa bao moja kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

Simba SC ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika na imekuwa na historia ndefu katika mashindano ya klabu barani Afrika. Safari yake katika mashindano ya mabingwa wa Afrika ilianza katika miaka ya 1970, wakati mashindano hayo yakijulikana kama African Cup of Champions Clubs.

Mwaka 1974 ulikuwa wa kihistoria kwa Simba baada ya kufika hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo. Hadi sasa, hiyo ni moja ya hatua za juu zaidi ambazo Simba imewahi kufikia katika historia yake ya mashindano ya klabu Afrika.

Katika miaka iliyofuata, Simba iliendelea kushiriki mashindano ya Afrika na kupata mafanikio mbalimbali.

Mwaka 2003, Simba iliandika historia nyingine baada ya kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya mabingwa Afrika.

Msimu wa 2018/19 ulikuwa mwingine wa kihistoria kwa Simba baada ya kufika robo fainali ya CAF Champions League, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kufikia hatua hiyo katika mfumo wa kisasa wa mashindano.

Simba ilifuzu baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi D nyuma ya Al Ahly SC.
Msimu wa 2020/21, Simba ilifanikiwa tena kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiendelea kujijengea heshima katika soka la bara la Afrika.

Msimu wa 2022/23, Simba ilifika tena robo fainali baada ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi. Katika mchezo muhimu, Simba iliichapa Horoya ya Guinea mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku mchezaji nyoto wa timu hiyo Clatous Chama akifunga hat-trick.

Msimu wa 2023/24, Simba ilifika t robo fainali na kukutana na mabingwa watetezi, Al Ahly SC. Simba ilipoteza kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kabla ya kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano mjini Cairo na kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0.

Historia ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika imekuwa ya mafanikio mbalimbali, kutoka kufika nusu fainali mwaka 1974 hadi kujenga utamaduni wa kufika hatua ya robo fainali katika miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo, hadi sasa Simba SC haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.