Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inaendelea kupiga hatua katika sekta za uwekezaji na utalii, hali inayozidi kuimarisha nafasi ya visiwa hivyo katika soko la utalii duniani.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 06 Septemba 2026, katika uzinduzi wa hoteli za Anaya Hotels & Resorts Zanzibar na Kappa Senses Zanzibar, zilizopo Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi na kufungua milango kwa wawekezaji ili wawe washirika muhimu wa maendeleo, huku ikihakikisha rasilimali na fursa zinazopatikana nchini zinawanufaisha wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema uwekezaji katika hoteli hizo umefikia zaidi ya dola za Marekani milioni 52, akieleza kuwa uwekezaji huo ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa imani ya wawekezaji kwa Serikali na mustakabali wa uchumi wa Zanzibar.
Ameeleza kuwa Zanzibar imefikia kiwango cha kupokea zaidi ya watalii laki moja kwa mwezi, hatua inayoongeza matumaini ya kufikia lengo la kupokea watalii milioni moja kwa mwaka.
Aidha, amesema uwekezaji huo tayari umezalisha ajira 371 kwa wananchi, zikiwemo ajira kwa wakaazi wa maeneo yanayozunguka miradi hiyo.
Amesema hoteli hizo pia zitatoa soko muhimu kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar, zikiwemo za kilimo, uvuvi na bidhaa nyingine za ndani, hatua itakayosaidia kuongeza fursa za biashara na kipato kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza viongozi wa Serikali, Wizara na taasisi zinazosimamia uwekezaji kwa juhudi za kuboresha mazingira ya biashara, akieleza kuwa matokeo yake yanaonekana kupitia ongezeko la miradi mikubwa ya uwekezaji nchini.
Amesema kuongezeka kwa idadi ya ndege zinazotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kunadhihirisha jinsi Zanzibar inavyoendelea kuvutia watalii na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kukuza utalii jumuishi, ambao manufaa yake yanamfikia mwekezaji, mtalii na mwananchi, ili ukuaji wa sekta hiyo uende sambamba na kuboreka kwa maisha ya wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wawekezaji wa hoteli hizo kwa kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara na wasanii wa sanaa za mikono kuonesha na kuuza bidhaa zao kwa watalii, jambo litakalosaidia kuongeza fursa za biashara na kipato kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu muhimu, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, umeme, maji na mawasiliano, ili kuwezesha shughuli za biashara, utalii na uwekezaji kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji, kutoa ushirikiano unaohitajika na kushughulikia changamoto zinazojitokeza, ili kuendelea kuimarisha sekta za utalii na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Naye, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, sambamba na kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji unaofanyika nchini.

