Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Mji wa Serikali Mtumba umeandaliwa kuwa na uwezo wa kuhudumia jumla ya watumishi 18,510.
Akizungumza Septemba 6, 2026 jijini Dodoma na waandishi wa habari, Prof. Kabudi, amesema kuwa majengo katika Mji wa Serikali Mtumba yamegawanywa kwa kuzingatia idadi ya watumishi watakaofanya kazi katika majengo hayo.
Amebainisha kuwa kuna aina mbalimbali za majengo, likiwemo jengo lenye uwezo wa kuchukua watumishi hadi 300, jingine hadi 500 na aina nyingine lenye uwezo wa kuchukua hadi watumishi 1,400.
Aidha, amesema majengo ya baadhi ya taasisi yameandaliwa kwa uwezo wa kuhudumia takribani watumishi 150, kulingana na mahitaji ya taasisi husika.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa mpangilio huo umezingatia mahitaji ya sasa ya Serikali pamoja na ongezeko la idadi ya watumishi katika siku zijazo.
Amesema kadri mahitaji ya nafasi za watumishi yatakavyoongezeka, Serikali itaendelea na hatua nyingine za utekelezaji ili kuhakikisha Mji wa Serikali Mtumba unakidhi mahitaji ya utendaji wa Serikali.

