Mkuu wa Mkoa mpya wa Mwanza, CP Salum Rashid  Hamdun (kushoto), na Said Mtanda (kulia), wakipongezane baada ya kubadilishana hati ya makabidhiano ya ofisi, leo.Mtanda amehamishiwa mkoani Simiyu kuchukua nafasi ya Anamringi Macha.
2-Mkuu wa Mkoa mpya wa Mwanza, CP Salum Rashid  Hamdun (kushoto), na Said Mtanda (kulia), wakionesha hati ya makabidhiano ya ofisi, leo.
3-Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Comred Christopher Ngubihagai akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), kwa niaba ya wakuu wa wilaya wenzake.

………….

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna wa Polisi (CP) Salum Rashid Hamdun, ameahidi kutumia nguvu, akili na weledi wake wote katika kutekeleza majukumu aliyopewa, akishirikiana na wananchi, watumishi wa umma na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mkoa huo unapata maendeleo.

CP Hamdun alitoa ahadi hiyo leo, wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya wananchi na watumishi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na kuanza majukumu yake kama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Alisema anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa dhamana hiyo na kwamba ataitumikia kwa uaminifu, uadilifu, weledi na uzalendo wa hali ya juu, huku akiahidi kuendeleza mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake, Said Mtanda.

“Leo naandika historia yangu kwa kukabidhiwa dhamana hii kubwa. Namshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Mkuu wa Mkoa,” alisema CP Hamdun.

Alisema anatambua ukubwa wa Mkoa wa Mwanza pamoja na changamoto zake, hivyo atahitaji ubunifu, msukumo na uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa viongozi, watumishi wa umma, wananchi na wadau mbalimbali ili kuzitatua.

“Ningependa kurejesha imani ya Rais kwa kufanya kazi. Nitahakikisha Mwanza inaendelea kuwa salama kwa kushirikiana na wananchi, ili watekeleze majukumu yao ya kijamii na kiuchumi wakiwa salama,” alisema.

Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, sera za Serikali na ahadi zilizotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni, CP Hamdun alisema atazisimamia na kuhakikisha zinatekelezwa kwa kasi, sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Alisema lengo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kufikia malengo makubwa yaliyowekwa katika dira hiyo.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, CP Hamdun alisema Mkoa utahakikisha mapato yanakusanywa kwa ufanisi huku wananchi wakielimishwa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari bila kulazimishwa.

Alisema mapato yatakayokusanywa yanapaswa kuelekezwa katika maeneo ya vipaumbele na miradi yenye manufaa kwa wananchi, huku matumizi yake yakizingatia thamani ya fedha, alisisitiza suala la usafi wa mazingira, akisema ni moja ya maeneo ambayo Serikali imeyapa uzito na kwamba Mwanza lazima iwe safi na salama.

“Maagizo ya Rais Dk. Samia wakati akituapisha Septemba 2, 2026, alielekeza na kusisitiza kuwa miji na mikoa yetu, ukiwemo Mwanza, ni michafu. Hii si sifa nzuri. Aibu hii tuhakikishe inatutoka, miji ibaki kuwa safi na salama,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiahagai, akizungumza kwa niaba ya wakuu wenzake wa wilaya, alisema wako tayari kushirikiana na Mkuu huyo mpya wa Mkoa katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Ngubiahagai alisema maelekezo ya CP Hamdun kuhusu usafi wa mazingira yanaendana na msisitizo wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa kuwa na mazingira safi ili kupunguza magonjwa na gharama za matibabu.

“Asilimia 60 ya magonjwa yanatokana na uchafu, hivyo Rais Samia anataka kila Mtanzania aishi katika mazingira bora ili apunguze gharama za matibabu,” alisema.

Ngubiahagai alisema viongozi wa wilaya wameagizwa kuwasikiliza wananchi, kutatua kero zao na kuwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa changamoto ambazo zinahitaji hatua za ngazi ya mkoa, lengo ni kutoa huduma bora kwa wananchi, wawe na tabasamu na waifurahie Serikali yao.

Alisema Rais anatekeleza ahadi zake kwa wananchi na kwamba kila kiongozi anapaswa kutumia rasilimali alizonazo kuhakikisha Mwanza inapata maendeleo na wananchi wanapatiwa ufumbuzi wa changamoto zao.

Ngubiahagai alisema pia Serikali inataka kuona ongezeko la mapato pamoja na matumizi sahihi ya fedha katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kunakuwa na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo.