NA FAUZIA MUSSA

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) zimeingia katika ushirikiano unaolenga kubadilisha namna soka la Zanzibar linavyoendeshwa, kutangazwa na kuwafikia mashabiki kupitia teknolojia za kidijitali.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuwezesha matumizi ya huduma za kidijitali katika soka, ikiwemo tiketi za kielektroniki, upatikanaji wa taarifa za michezo na kuimarisha usimamizi wa mapato ya mechi.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Riziki Pembe Juma, alisema teknolojia imekuwa sehemu muhimu ya uendeshaji, ufuatiliaji na utangazaji wa michezo. 

Alisema ushirikiano huo utaiwezesha soka la Zanzibar kufikia hadhira pana zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, huku mashabiki wakipata taarifa kuhusu ratiba, matokeo, timu, wachezaji na mashindano kwa urahisi na kwa wakati.

“Mafanikio ya ushirikiano huu yatapimwa siyo kwa kusainiwa kwa mkataba pekee, bali kwa matokeo utakayoleta kwa maendeleo ya soka na matumizi ya teknolojia Zanzibar,” alisema Dkt. Pembe

Dkt. Pembe alisema matumizi ya teknolojia yanaweza pia kuongeza mwonekano wa vipaji vya vijana, wachezaji, vilabu na mashindano ya Zanzibar, hatua ambayo inaweza kufungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji, udhamini na ajira katika sekta ya michezo.

Waziri huyo aliipongeza ZFF kwa kuanza kutumia mfumo wa N-CARD katika tiketi za kielektroniki, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuondokana na matumizi ya tiketi za karatasi na kuboresha ufanisi, usalama na udhibiti wa mapato katika matukio ya michezo. 

Alisema mfumo huo unapaswa kutumiwa kwa ufanisi na kufanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya mashabiki na wadau wa michezo.

” teknolojia katika michezo haipaswi kuishia kwenye tiketi pekee, bali itumike pia katika matangazo, maudhui ya michezo, huduma kwa mashabiki, biashara ya bidhaa za timu na udhamini. ” Alisema 

Aliwataka TTCL na ZFF kuweka mpango madhubuti wa utekelezaji wenye malengo na muda maalumu, kuhakikisha huduma za kidijitali zinakuwa rahisi kwa mashabiki, pamoja na kuzingatia usalama wa taarifa na miamala ya kidijitali.

Aidha, aliwataka kuwajengea uwezo watendaji wa michezo kutumia teknolojia na kuwapa nafasi vijana wenye vipaji vya teknolojia kushiriki katika mifumo hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, alisema ushirikiano huo unalenga kuwezesha upatikanaji wa intaneti na suluhisho mbalimbali za kidijitali zitakazoboresha shughuli za ZFF na kuongeza ushiriki wa mashabiki katika matukio ya michezo.

Alisema matumizi ya N-CARD yatawawezesha mashabiki kununua na kuthibitisha tiketi kwa urahisi, huku ZFF ikiweza kusimamia mahudhurio na mapato kwa uwazi zaidi.

Mwita alisema mfumo huo pia utawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu mapato yanayotokana na sekta ya michezo, huku akieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kusaidia kuipeleka soka la Zanzibar katika majukwaa ya kimataifa ya kidijitali.

Naye, Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za shirikisho hilo kubadilisha mifumo yake ya uendeshaji ili kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soka la kisasa.

Vuai alisema ZFF imepanga kuendeleza mabadiliko hayo kwa kuanzisha huduma mbalimbali za kidijitali, ikiwemo ZFF TV na ZFF App, ambazo zinalenga kuboresha namna shirikisho hilo linavyowasiliana na kutoa huduma kwa jamii.

Alisema utekelezaji wa mipango hiyo unahitaji ushirikiano na taasisi za mawasiliano pamoja na wadau wengine wa teknolojia ili kuimarisha mifumo ya mawasiliano na huduma za kidijitali ndani ya shirikisho.

Alisema mageuzi hayo yana umuhimu zaidi wakati Zanzibar ikiendelea kuimarisha miundombinu ya michezo na kushiriki katika maandalizi ya matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo AFCON 2027.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa ZFF, Awadh Maulid Mwita, alisema shirikisho limeamua kurasimisha na kuimarisha ushirikiano na wadhamini na wafadhili mbalimbali kwa lengo la kuendeleza soka Zanzibar.

Alisema mifumo ya kidijitali itaongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato, ikiwemo kutoa taarifa kuhusu mapato ya mechi, idadi ya mashabiki wanaoingia viwanjani na mwenendo wa shughuli mbalimbali za shirikisho.

Alisema uzoefu wa awali katika mchezo wa Ngao ya Jamii umeanza kuonyesha manufaa ya mfumo huo, ikilinganishwa na utaratibu wa zamani wa kutumia madaftari na risiti ambao ulikuwa na changamoto katika udhibiti na ufuatiliaji wa mapato.