Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikipata maelezo ya kifaa cha upimaji kutoka kwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo Cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Sabrina Guga (Kushoto) wakati Kamati hiyo ilipokwenda kukagua miradi ya chuo hicho Agosti 30, 2026 mkoani Morogoro.
Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili kada ya Mipango Miji katika Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Caroline Gebron Materu (Kulia) akielezea Mpango wa Uendelezaji eneo la Gezaulole mkoani Lindi ulioandaliwa na chuo hicho kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipokwenda chuoni kukagua miradi ya chuo Agosti 30, 2026 mkoani Morogoro.
Mkuu wa chuo Cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Bw. Charles Saguda akielezea Mpango Kabambe wa Uendelezaji Chuo cha ARIMO katika eneo la Mlimakola mkoani Morogoro kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Agosti 30, 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
…………….
Na Munir Shemweta, MOROGORO
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mzava, ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza nguvu katika kuboresha na kupanua Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) ili kuongeza uwezo wa kuzalisha wataalamu wengi zaidi katika sekta ya ardhi.
Aidha, Mhe. Mzava ameitaka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Upangaji) katika kuweka utaratibu wa kutumia wataalamu wanaozalishwa na vyuo vya ardhi kusaidia wananchi kutatua changamoto za ardhi na hivyo kupunguza migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Mzava ametoa kauli hiyo, Agosti 30, 2026, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO), mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mzava amekipongeza Chuo cha Ardhi Morogoro kwa kazi kinayoifanya ya kuwaandaa vijana kitaaluma licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Nikipongeze Chuo cha Ardhi Morogoro. Pamoja na changamoto zake, kinafanya kazi nzuri ya kuwaandaa vijana ili watumikie Taifa lao.”
Amesema, chuo hicho ni taasisi muhimu katika uzalishaji wa wataalamu wa sekta ya ardhi na kwamba ni muhimu kuendelea kuboresha mipango yake ya maendeleo, ikiwemo kutekeleza mpango kabambe wa chuo.
Amebainisha kuwa, anatamani kuona mabadiliko makubwa katika vyuo vya Ardhi vya Morogoro na Tabora, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu, mazingira ya kujifunzia na uwezo wa vyuo hivyo kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kutembelea Chuo cha ARIMO na kujionea shughuli zinazofanyika katika chuo hicho.
Waziri Akwilapo ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa Wizara yake itakiangalia kwa karibu Chuo cha Ardhi Morogoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea na kujifunzia.
Nao wajumbe wa Kamati wamekipongeza Chuo cha Ardhi Morogoro na Wizara kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuendeleza elimu ya ardhi nchini.
Hata hivyo, wamependekeza chuo kuangalia uwezekano wa kuongeza na kuanzisha kozi mbalimbali tofauti na zile zinazotolewa kwa sasa, ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza fursa kwa vijana.
Wajumbe hao pia wamekishauri chuo kuanza mapema kutafuta maeneo ya ardhi kwa ajili ya upanuzi wa shughuli zake katika miaka ijayo, wakieleza kuwa si jambo baya kwa chuo kutafuta eneo katika mikoa mingine, ikiwemo Iringa, kwa ajili ya shughuli za kitaaluma na maendeleo ya chuo.
Vile vile wamesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa lengo la kusaidia wanafunzi kupata mafunzo yanayozingatia teknolojia za kisasa na kuwawezesha kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Katika ziara yake ya siku moja katika Chuo cha Ardhi Morogoro Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipata taarifa maendeleo ya chuo Pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa Pamoja mpango wa uendelezaji chuo katika eneo la Mlimakola mkoani Morogoro.
