Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Joseph Mkude akizungumza kwenye baraza hilo jijini Arusha leo .
…………
Na Happy Lazaro, Arusha .
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewataka wananchi na viongozi jijini humo kuweka maslahi ya umma mbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa changamoto zinazoweza kujitokeza hazipaswi kutumiwa kama sababu ya kusimamisha miradi yenye manufaa kwa jamii.
Mkude ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika Baraza la Madiwani la halmashauri ya Jiji la Arusha, na kusema kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu na huduma muhimu kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa viongozi katika ngazi mbalimbali kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema baadhi ya miradi mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa Arusha inalenga kwenda sambamba na mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa jiji, huku akiwataka Madiwani kuwa sehemu ya kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa vizuri na kukamilika kwa wakati.
“kumekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo yanayopitiwa na miradi, hivyo nawataka wananchi wanaohusika kushirikiana na Serikali ili kupata ufumbuzi wa masuala yanayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.”amesema Mkude.
Amesisitiza kuwa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wengi inapaswa kupewa kipaumbele, badala ya kuruhusu maslahi ya mtu au kundi dogo kuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii.
Mkude ameongeza kuwa, viongozi wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa miradi hiyo na kuhakikisha mawasiliano yanafanyika kwa wakati ili changamoto zinazojitokeza zisigeuke kuwa sababu ya kuchelewesha utekelezaji.
Mbali na miundombinu, Mkude amesisitiza umuhimu wa usafi katika Jiji la Arusha, akisema hali ya mazingira inapaswa kuwa sehemu ya ajenda ya kila siku ya viongozi na wananchi.
Amepongeza kazi zinazofanywa na Madiwani, Mstahiki Meya pamoja na vikundi vinavyoshiriki katika usafi wa jiji, lakini akasema juhudi hizo zinahitaji kuongezwa ili kuhakikisha maeneo yote ya jiji yanakuwa katika hali nzuri.
Kwa upande wa wananchi, amewataka kubadilisha mtazamo kuhusu utunzaji wa mazingira kwa kuhakikisha taka zinatupwa katika maeneo yaliyotengwa na kushiriki kikamilifu katika kulinda usafi wa maeneo yao.
Mkude amesema Arusha inapaswa kujiweka katika mazingira bora zaidi kutokana na nafasi yake ya kuwa mwenyeji wa mikutano na matukio mbalimbali ya kimataifa, hali inayofanya usafi na mwonekano wa jiji kuwa sehemu ya taswira ya Tanzania.
Ametaja maandalizi ya mkutano wa Bunge la Dunia (IPU) unaotarajiwa kufanyika Arusha mwezi Oktoba kuwa fursa muhimu kwa jiji hilo kuendelea kujitangaza kimataifa na kuonyesha uwezo wake wa kupokea wageni wa kimataifa.
Amesema maandalizi ya matukio hayo yanapaswa kuhusisha viongozi, wananchi na taasisi mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu, mazingira na usalama wa jiji.
Mkude amewataka wakazi wa Arusha kuendelea kushirikiana na Serikali katika masuala ya maendeleo, akisema mafanikio ya jiji hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee bali yanahitaji ushiriki wa kila mmoja.

