Na. Joseph Mahumi, Dar es Salaam
Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), Mhe. Dkt. Martin Kolikoli, amewataka wadau hususan wawekezaji kulitumia Baraza lake ili kutatua migogoro ya biashara kwa uharaka zaidi kwa lengo la kuchochea uwekezaji, biashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Dkt. Kolikoli ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika Ofisi za Baraza la Ushindani (FCT) jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu na mbinu bora katika uendeshaji na usimamizi wa mashauri, hususan matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Alisema ziara hiyo imelenga kujifunza kutoka FCT ambayo ina uzoefu mkubwa katika kushughulikia migogoro, ambapo katika kipindi cha miaka 20 imepokea na kutatua zaidi ya mashauri 500, ikiwemo migogoro inayohusisha ushindani wa kibiashara, huku kwa upande wa CMT, amesema baraza hilo limeanza kutekeleza majukumu yake takribani miaka mitatu iliyopita na tayari limepokea mashauri mbalimbali na kusajili migogoro sita.
Dkt. Kolikoli alisema uzoefu huo ni muhimu kwa CMT kwa kuwa unaliwezesha kujifunza mifumo na mbinu zinazotumika na taasisi yenye uzoefu zaidi, ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu yake, huku likiboresha huduma kwa wananchi na wadau wa masoko ya mitaji na bidhaa.
Aidha, alisema moja ya maeneo ambayo Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), inalenga kujifunza ni namna ya kupanga na kusimamia mashauri kwa ufanisi, kwa kuwa mfumo mzuri wa usimamizi wa mashauri unaweza kusaidia kupunguza mrundikano wa kesi na kuhakikisha migogoro inatatuliwa ndani ya muda unaostahili.
“Lengo la kuwa na mabaraza haya yenye hadhi sawa na Mahakama Kuu ni kurahisisha utatuzi wa migogoro kama jambo linaenda mahakamani, linaweza kuchukua muda mrefu, lakini kupitia Baraza tunaweza kuhakikisha linatatuliwa kwa muda mfupi zaidi,” alisema Dkt. Kolikoli.
Alieeleza kuwa kwa mujibu wa taratibu za Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), mashauri yanapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 90 pekee, hivyo kujifunza namna FCT inavyopanga, kusajili na kusimamia mashauri kutasaidia CMT kuimarisha mifumo yake na kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa wakati, kwa kuwa ndiyo Taasisi inayowahudumia wawekezaji na wadau mbalimbali wa masoko ya mitaji na bidhaa, ina wajibu wa kuhakikisha migogoro inayojitokeza inatatuliwa kwa haki na kwa muda mfupi ili kujenga imani katika masoko hayo.
Aliongeza kuwa wigo wa wadau wanaonufaika na huduma za CMT ni mpana na unahusisha wawekezaji, mabenki, mawakala wa masoko, kampuni zilizoorodheshwa katika soko la hisa pamoja na washiriki wa soko la bidhaa, wakiwemo wakulima, wanachama wa vyama vya ushirika (AMCOs), waendeshaji wa maghala na wafanyabiashara wanaonunua bidhaa zinazouzwa kupitia masoko ya bidhaa.
Dkt. Kolikoli alisema utatuzi wa migogoro kwa wakati ni muhimu zaidi katika masoko ya bidhaa kwa sababu kuchelewa kwa uamuzi kunaweza kusababisha hasara kubwa kwa wahusika.
Alisema bidhaa inaweza kubaki imehifadhiwa katika ghala kwa muda mrefu kutokana na mgogoro na hatimaye kupoteza ubora au thamani yake.
“Bidhaa ikiwa imefungiwa ndani ya maghala kwa sababu ya mgogoro na kesi ikachukua miaka mingi mahakamani, bidhaa hiyo inaweza isifae tena, lakini kupitia baraza, ndani ya muda mfupi, muhusika anaweza kupata haki yake,” alisema Dkt. Kolikolo.
Aidha, alisema kasi ya utatuzi wa migogoro ni muhimu pia katika sekta ya fedha kwa sababu fedha zinapokuwa zimefungwa kwa muda mrefu haziwezi kutumika katika shughuli za kiuchumi na thamani yake inaweza kuathirika.
Aliongeza kuwa kadri soko la mitaji na bidhaa linavyoendelea kukua, ndivyo umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa utatuzi wa migogoro unavyoongezeka, na ongezeko la idadi ya washiriki katika soko la hisa pamoja na kukua kwa thamani ya jumla ya soko (market capitalisation) ni viashiria vya ukuaji wa soko, hivyo mifumo ya kulinda haki za wawekezaji na wadau wengine inapaswa kwenda sambamba na kasi hiyo.
Dkt. Kolikoli alisema Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT) litaendelea kushirikiana na taasisi zenye uzoefu, ikiwemo FCT, ili kujenga uwezo wa watendaji, kuboresha mifumo ya kidijitali na kuhakikisha huduma za utatuzi wa migogoro zinapatikana kwa ufanisi, uwazi na kwa wakati.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Ushindani (FCT), Mhe. Mbegu Kaskasi, alisema Baraza hilo limeanzishwa chini ya Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 kwa jukumu la kusikiliza na kutatua migogoro inayohusu biashara na ushindani, pamoja na kulinda haki za walaji kupitia mfumo wa rufaa na moja ya majukumu makuu yake ni kusikiliza rufaa zinazotokana na Tume ya Ushindani (FCC), pamoja na rufaa kutoka kwa mamlaka mbalimbali za udhibiti katika sekta zinazohusiana na shughuli za biashara.
Mhe. Kaskasi alisema ziara ya Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT) imekuwa fursa muhimu kwa taasisi hizo mbili kubadilishana uzoefu katika usimamizi na utatuzi wa mashauri, huku akieleza kuwa licha ya FCT kuwa na uzoefu wa takribani miaka 20 na CMT kuwa ni chombo kilichoanzishwa miaka michache iliyopita, kila taasisi imeweza kujifunza kutoka kwa nyingine.
“Tangu kuanzishwa kwake FCT imeshughulikia jumla ya mashauri 525, huku ikipokea wastani wa mashauri kati ya 45 na 50 kwa mwaka, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kuimarisha uwezo wa Baraza kadri shughuli za biashara na uwekezaji zinavyoongezeka nchini” alisema Mhe, Kaskasi
Aliongeza kuwa baadhi ya mashauri yana thamani ya fedha inayoweza kupimika moja kwa moja, wakati mengine yana athari kubwa kiuchumi ambazo si rahisi kuzitafsiri kwa thamani ya fedha, akitoa mfano wa mashauri yanayohusu uunganishaji na ununuzi wa kampuni (mergers and acquisitions), ambapo miamala inaweza kuhusisha hisa zenye thamani ya matrilioni ya fedha.
Mhe. Kaskazi alisema ushirikiano wa FCT na CMT utaendelea ili kuwezesha mabaraza hayo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha migogoro ya biashara inatatuliwa kwa muda mfupi, badala ya kuendelea kwa muda mrefu katika mfumo wa mahakama, jambo linaloweza kuchelewesha shughuli za wafanyabiashara na uwekezaji.

