Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kusambaza huduma za matibabu ya saratani katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Agosti 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Welezo, Mhe. Asma Ali Mwinyi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kuhusu mpango wa Serikali wa kusambaza huduma za ORCI katika mikoa mingine nchini.
Amesema katika kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa huduma za matibabu ya saratani katika Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkapa, ambapo mradi huo umefikia asilimia 80 kwa gharama ya shilingi bilioni 28.9.
Aidha, amesema ujenzi wa mradi wa huduma za saratani katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya umefikia asilimia 60 kwa gharama ya shilingi bilioni 10, huku miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika Januari, 2027.
Dkt. Samizi ameongeza kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya ujenzi wa bunkers za mashine za mionzi katika Hospitali ya Kanda ya KCMC na Bugando, ambapo huduma za matibabu zimeanza kutolewa na kuziwezesha hospitali hizo kuwa na uwezo timilifu wa kutoa tiba ya mionzi na dawa kwa wagonjwa wa saratani.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za kibingwa za saratani zinawafikia wananchi karibu na maeneo wanayoishi na hivyo kupunguza gharama na changamoto za wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi, ambapo zaidi ya vituo 1,760 kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa vimewezeshwa kutoa huduma hizo.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za saratani katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uchunguzi, matibabu na rufaa kwa wakati na kwa urahisi zaidi.

