Washington Dc,
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewasili katika Ubalozi wa Tanzania jijini Washington D.C., Marekani, leo Agosti 26, 2026, na kupokelewa na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Bi. Eva Ng’itu.
Mhe. Ndejembi yuko Washington D.C. kushiriki katika Kikao cha Ngazi ya Mawaziri cha Uzinduzi wa Mpango wa Atomic Technologies Licensed for Applications at Sea (ATLAS), kinachofanyika tarehe 26 na 27 Agosti 2026.
Mpango wa ATLAS ni mpango mpya wa International Atomic Energy Agency (IAEA) unaolenga kuendeleza matumizi salama, yenye ulinzi na endelevu ya teknolojia za nyuklia katika shughuli za baharini, ikiwemo matumizi ya meli zinazotumia nishati ya nyuklia pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme wa nyuklia inayoelea baharini.
Kikao hicho ni muhimu na cha kimkakati kwa Tanzania, ikizingatiwa kuwa nchi ipo katika hatua za awali za maandalizi ya Programu ya Umeme wa Nyuklia. Ushiriki wa Tanzania unatoa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo ya teknolojia za nyuklia, ikiwemo Small Modular Reactors (SMRs), pamoja na mifumo ya kisheria, kisera, kiudhibiti, kiusalama na kitaasisi inayohitajika katika kuhakikisha matumizi salama na yenye ufanisi ya teknolojia hizo.
Mhe. Ndejembi ameambatana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Simon Songe, Wajumbe wa Kamati hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

