Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, akiwa na maofisa, wakaguzi na askari, aliwaongoza askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe katika kusherehekea miaka 20 ya Polisi Jamii kwa kufanya matendo ya huruma kwa familia ya Bi. Enitha Sinyinza iliyopo Kijiji cha Hezya, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Hezya tarehe 26 Agosti 2026, Kamanda Senga amewataka kuwa karibu na Jeshi la Polisi na kushirikiana katika kuzuia na kupambana na uhalifu, akisisitiza kuwa usalama hauwezi kulindwa na Jeshi la Polisi pekee bila ushirikiano wa wananchi. Aidha, amewataka wananchi hao kuachana na imani za kishirikina kwa kuwa zinaweza kusababisha migogoro na kuvuruga amani ndani ya familia na jamii.

Baada ya kuzungumza na wananchi, Kamanda Senga alielekea nyumbani kwa Bi. Enitha Sinyinza, mwenye watoto watano ambao wote wana changamoto ya ugonjwa wa usonji, ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe lilimpatia msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya familia hiyo.

Aidha, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi Maria Kway, amempongeza Bi. Enitha kwa moyo na uvumilivu mkubwa aliouonesha katika kuwalea na kuwatunza watoto wake, akisema mama huyo ni “Malkia wa Nguvu” kutokana na namna anavyoipambania familia yake licha ya changamoto anazokabiliana nazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Hezya, Lamsoni Mwashilindi, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa hatua hiyo ya huruma, akisema msaada huo ni mkubwa na wa kuigwa kwani familia hiyo inakabiliwa na changamoto za kiafya pamoja na mahitaji mbalimbali ya kila siku.