Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Mha. Zena Ahmed Said amefanya kikao na wadau wa sekta ya ajira ili kuongeza fursa za ajira, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na ushindani wa Watanzania katika soko la ajira nchini Saudi Arabia na Mashariki ya Kati.
Aidha, Balozi Zena amefanya kikao hicho ili kutambua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo mawakala hao, mchakato mzima wa kuwasajili Watanzania wanaopata ajira Saudi Arabia na changamoto wanazokabiliana nazo ugenini.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala Binafsi wa Ajira (TRAA), Bw. Abdallah Mohammed ameipongeza Serikali kwa jitihada za kuendelea kufungua milango ya upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi kwa Watanzania. Pia ameeleza kuwa ili kuboresha mazingira ya Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi, ni muhimu kwa Serikali kushiriki katika majadiliano ya mara kwa mara na mataifa hayo.
Ikumbukwe kuwa, Mashariki ya Kati ni soko kubwa zaidi la ajira kwa Watanzania nje ya nchi.

