Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha inatumia ipasavyo gari la wagonjwa (ambulance) lililokabidhiwa na Serikali, ili kuongeza ufanisi wa huduma za dharura na rufaa kwa wananchi badala ya kutumika katika safari binafsi ama matumizi yasiyo husiana na huduma za afya.

Aidha ameelekeza magari mengine yenye changamoto za ubovu mbalimbali zitengenezwe ili yaendelee kusaidia kutoa huduma.

Mchengerwa ametoa agizo hilo Agosti 24, 2026, wakati akikabidhi ambulance hiyo yenye thamani ya sh milioni 105 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Mlandizi mkoani Pwani.

Nae Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuboresha sekta ya afya amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuongeza miundombinu, dawa, vifaa tiba sanjali na kulitumikia Taifa ili kuinua maendeleo na uchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameeleza kuwa Pwani kwa sasa ina zaidi ya vituo 635 vya afya, huku upatikanaji wa dawa katika mkoa huo ukifikia wastani wa asilimia 80.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Dkt. Wilford Kondo, amesema , katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Halmashauri hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya afya, hatua iliyosaidia kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali.