Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza leo Agosti 24, 2026 kwenye ziara ya kikazi mkoani Manyara
………..
Na Happy Lazaro, Arusha.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameagiza kuimarishwa kwa utafiti wa madini ya Tanzanite katika eneo la Mererani ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha rasilimali hiyo adimu inaendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Mavunde ametoa agizo hilo leo  baada ya kutembelea mgodi wa Franone Mining &Gem Co  Ltd uliopo Kitalu C, Mererani, wilayani Simanjiro mkoani  Manyara, ambako amekagua shughuli za uchimbaji na kuona hatua zinazochukuliwa na kampuni hiyo katika kuendeleza uzalishaji wa Tanzanite.
Amesema bado kuna fursa kubwa ya kugundua maeneo mengine yenye akiba ya Tanzanite endapo utafiti wa kina utafanyika kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Aidha ameitaka kampuni.hiyo ya  Franone kuongeza uwekezaji katika utafiti badala ya kutegemea maeneo ambayo tayari yamefanyiwa uchimbaji.
“Lazima tuongeze utafiti katika maeneo yetu ya Tanzania. Imani yangu ni kwamba tukifanya utafiti wa kutosha katika eneo hili la Tanzanite, tunaweza kufanya vizuri zaidi,” amesema Mavunde.
Amesema Serikali tayari imeweka mazingira ya kuimarisha utafiti wa madini nchini kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa katika sekta ya madini kwa ajili ya shughuli hizo, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa Taifa kugundua na kuthamini rasilimali zilizopo chini ya ardhi.
Mbali na kusisitiza utafiti, Mavunde amezindua matumizi ya kofia maalumu zenye teknolojia inayowawezesha watumiaji kuona na kufuatilia mazingira ya ndani ya migodi, akisema ubunifu huo unaweza kuwa sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya wizi na utoroshaji wa Tanzanite.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kusaidia kuongeza ulinzi, usalama na udhibiti wa shughuli zinazofanyika ndani ya migodi, huku yakirahisisha ufuatiliaji wa maeneo ambayo yanaweza kuwa na mianya ya upotevu wa madini.
Mavunde amesisitiza kuwa Serikali haitaki teknolojia itumike kwa ajili ya kuongeza uzalishaji pekee, bali pia kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia sheria, huku maslahi ya Taifa yakipewa kipaumbele.
Kwa upande mwingine, ameitaka kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika shughuli za uchimbaji, akieleza kuwa sekta ya madini inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wawekezaji ili kuongeza manufaa kwa Taifa.
Aidha Mavunde ameipongeza kampuni ya  Franone Mining  &Gem Co .Ltd kwa kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji, akisema hatua hiyo imefungua fursa za ajira na kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini.
Aidha, amepongeza uwekezaji unaofanywa na kampuni hiyo pamoja na mchango wake katika jamii inayozunguka mgodi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa huduma za kijamii kupitia ujenzi wa zahanati.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kuongeza thamani ya Tanzanite na madini mengine yanayopatikana nchini, ili Tanzania isibaki kuwa nchi yenye rasilimali pekee, bali iweze kunufaika zaidi kiuchumi kupitia uzalishaji, usimamizi na matumizi sahihi ya madini hayo.